
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amewasimamisha kazi, Meneja wa Wakala wa Huduma za Maji Mjini na Vijijini Mkoa wa Mara (RUWASA) Sadick Chakka na Meneja wa RUWASA Wilaya ya Tarime, Marwa Murasa kwa kushindwa kusimamia utekelezaji wa Miradi ya maji.
Waziri Aweso pia amemuagiza Katibu Mkuu wa WIzara ya Maji, Antony Sanga kutengua uteuzi zao kwa kuwa zipo kazi nyingi Wizarani za kufanya. Ametoa maagizo hayo Januari 5 alipokuwa anakagua Mradi wa Maji wa Magoto.

“Nataka mabadiliko Mara, miradi ya maji ikamilike kwa wakati, wananchi wapate maji. Faraja yangu ni kuona wananchi wanapata maji kila sehemu ndio maana tulianzisha wakala wa maji vijijini. Kwanini watu hawana maji manachezeachezea fedha, tulibainisha mikoa 17 na tulileta sh. Bilioni 119 na Mara peke yake tulileta bilioni 8 na bado watu hawapati maji,” amesema Aweso.

Ameongeza kuwa, Mradi wa Maji aliotembelea ulikuwa hautoi maji ambapo Serikali ilipeleka zaidi ya Tsh. Bilioni 8 kwa Miradi ya Maji ya Mkoa wa Mara na fedha zilizobaki hadi sasa ni Tsh. bilioni 3 hivyo ameona hawana kisingizio cha msingi.

Waziri amesema, tathmini aliyoifanya inaonyesha miradi mingi imekamilika kwa zaidi ya asilimia 90 lakini haitoi maji na hivyo aliwataka wataalam kote nchini kutumia vyema utaalamu wao badala ya kujiamulia kujenga miradi kiholela.