×

Wananchi Wasema Viongozi Wamekopeshana Saruji ya Zahanati Buchosa – Video

WANANCHI wa Kijiji cha Kasheka, Kata ya Bangwe katika Jimbo la Buchosa, Wilaya ya Sengerema, mkoani Mwanza,  wamecharuka baada ya viongozi wa serikali ya kijiji hicho kutuhumiwa kwa matumizi mabaya ya vifaa vya ujenzi vinavyoletwa kijijini hapo kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho.

 

 

Wakizungumza wakati wa mkutano wa hadhara na Mbunge wa Jimbo hilo, Mhe. Eric Shigongo, wananchi hao wamedai kuwa viongozi wa kijiji wamekopeshana mifuko 200 ya saruji ambayo ililetwa kwa ajili ya ujenzi wa zahanati hiyo na mpaka sasa hakuna aliyerudisha.

 

 

“Tunakushukuru Mhe. Mbunge kwa kutuletea mifuko 100 ya saruji, ile zahati imechukua mifuko 250, ukiongeza na ya kwako inakuwa 350, jiandae kutoona chochote pale, usipokuwa makini viongozi wa Serikali ya Kijiji watagawana hiyo mifuko na zahanati haitokamilika.

 

 

“Kuna mifuko ilitolewa pale, viongozi wamekopeshana, wamekuwa na tabia hiyo kwa muda mrefu, mtaendelea kutusaidia mpaka lini?   Pia, kuna viongozi wa kata ukienda ofisini na shida wanakutoza Tsh 5,000 inakwenda wapi?” amesema Mzee Adam Mafuru Malogo.

 

 

Naye Mhe. Shigongo amewaambia wananchi kwamba mbunge wao ni mjasiriamali, anafahamu machungu ya kutafuta pesa na matumizi mabaya ya pesa.

 

 

“Saruji hii imetoka kwa mjasiriamali, ikipotea hata punje moja ya saruji tusilaumiane, ole wao waitumie vibaya hiyo saruji, wote wataishia Gereza la Kasungamile na hii tabia ya kula mali za umma katika jimbo hili imefika mwisho, ambao wanabisha wajaribu waone,” amesema Shigongo.

 

Leave a Comment