
WAZIRI wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi, anatarajiwa kuwasili nchini Tanzania leo Alhamisi, Januari 7, 2020, kwa ziara ya siku siku mbili inayotarajiwa kuendeleza mahusiano ya biashara na diplomasia baina ya mataifa hayo.
Yi yupo katika ziara maalumu barani Afrika akimwakilisha rais wa nchi hiyo yenye uchumi mkubwa wa pili duniani. Anatarajiwa kuwasili mkoani Geita hii leo na kufanya mazungumzo na Rais John Magufuli.
China ni moja ya nchi zenye uwekezaji mkubwa wa moja kwa moja nchini Tanzania ambao unakia dola bilioni 7.5. Kwa mujibu wa Msemaji wa Serikali ya Tanzania, makampuni ya China yamewekeza takriban miradi 950 nchini humo.
Hata hivyo, miaka ya karibuni imeshuhudia baadhi ya miradi mikubwa ambayo nchi hizo mbili zilitarajiwa kuifanya ikichelewa ama kushindikana kwa kile wachambuzi wanasema ni Tanzania kuona maslahi yake yataminywa kwa masharti yaliyokuwapo mezani.
Mazungumzo juu ya mradi wa Bandari ya Bagamoyo ni moja ya miradi iliyokwama. Awali ilitarajiwa kuwa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge pia ungetekelezwa kwa mkopo kutoka Uchina, lakini serikali ya Magufuli ilianza ujenzi huo kwa fedha za ndani na kutumia kampuni ya ujenzi kutoka Uturuki.
Hata hivyo, waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi, ameeleza kuwa ujenzi wa reli hiyo kwa awamu ya tano utakuwa sehemu ya ajenda ya ziara hiyo. China na Tanzania zimekuwa na mahusiano imara kwa zaidi ya miaka 50 sasa. Ziara ya Yi pia imehusisha nchi za Nigeria, DRC, Botswana na Ushelisheli.