
WATU wawili wamenusurika kifo baada ya basi la Pollman Tours na Safari Company walilokuwa wamepanda kuteleza na kuzama baharini katika Kivuko cha Likoni, Mjini Mombasa, Kenya, mapema jana.
Manusura hao waliokolewa na watu waliokuwa karibu na eneo la tukio. Polisi la Mombasa imethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa eneo hilo huwa na utelezi mkubwa pindi mvua zinaponyesha.
GVazeti la Nation, limeandika kuwa basi liliteleza kutoka kwenye feri na kutumbukia baharini majira saa nne asubuhi Dereva na kondakta waliokolewa wote na polisi na walinzi wa kivuko.
Basi hilo la Yutong luxury lilikuwa linatokea Diani ambapo lilikuwa limewapeleka watalii waliowasili Mombasa.
Dereva wa basi hilo, Salim Omar, aliwaambia polisi kuwa alishindwa kulidhibiti gari hilo baada kuanza kuteleza, na kulikuwa na mvua iliyonyesha majira ya asubuhi.
“Nilikuwa karibu nafika feri lakini basi likanizidi nguvu na kutumbukia baharini, Ninamshukuru tu Mungu kuwa tuko salama,” alisema.