×

Mfanyabiashara Adai Kuporwa Eneo Alilonunua na Aliyemuuzia

Nicodemu Mollel akizungumza na Global Tv.

MFANYABIASHARA Nicodemus Mollel mkazi wa Zanzibar amemshutumu Bwana Silvester mkazi Kijiji cha Msolwa Kata ya Kisanga Wilayani Kilosa mkoani Morogoro kwa kumuuzia nyumba na eneo la wazi na kisha kumpora eneo hilo la wazi na kujenga mwenyewe.

Akizungumza na mwandishi wetu Nicodemus amesema awali aliinunua nyumba hiyo iliyopo Kijiji cha Msolwa ikiwa na eneo la wazi kwa shilingi milioni 11.

Nicodemus amesema baada ya kumlipa pesa yote aliyemuuzia alisafiri lakini aliporudi ghafla alikuta aliyemuuzia amejenga nyumba ya kuishi kwenye eneo alilonunua.

“Nilipoona hivyo nilimshangaa sana aliyeniuzia ndipo nikaamua kumfuata na kumuuliza lakini cha ajabu akaanza kuniruka na kusema eti hakuniuzia hilo eneo alichoniuzia ni nyumba na si eneo alilojenga.

“Hapo nilianza kuhangaikia haki yangu kwa kufuata sheria ambapo mpaka sasa bado sakata hilo linaendelea hivyo nawaomba Viongozi wa serikali na Wasamaria wema wengine mnisaidie kupata haki yangu”. Aliomba msaada Nicodemus na kutaja namba yake 0786536140 kwa yeyote anayeweza kumsaidia.

Kufuatia sakata hilo mwanahabari wetu alikwenda mpaka kijijini hapo na kukutana na Afisa Mtendaji wa kijiji hicho aliyejitambulisha kwa jina la Patricia Kimbuli.

Afisa Mtendaji wa Kata ya Kisanga, Patricia Kimbuli akizungumza na Global Tv.

Akizungumza na mwanahabari wetu Patricia alisema analifahamu sakata hilo ingawa lilianza kabla hajaingia madarakani amelikuta na ameshawahi kulifanyia kazi.

“Hilo sakata nalifahamu ila hapa kwenye nafasi hii mimi ni mgeni ila nililikuta na nimeshawahi kulifanyia kazi.

“Nakumbuka hivi karibuni nilipigiwa simu na bosi wangu Mkuu wa Wilaya ya Kilosa ambaye aliniulizia kuhusu mgogoro huo na kuniambia nikafanye uchunguzi kisha nimpelekee majibu.

“Nami nilifanya kama alivyoniagiza nikaenda eneo la tukio nikaliangalia na kumuuliza Silvester kwanini alikuwa amejenga kwenye eneo alilomuulizia Nicodemus lakini alinijibu kuwa eneo hilo alilojenga siyo alilomuuzia.

Nicodemu akiwa kwenye sehemu ya nyumba aliyouziwa.

“Aliniambia eneo alilomuuzia ni eneo la nyumba na sehemu fulani ambayo amenionesha lakini siyo mpaka eneo alilojenga.

“Wakati muuzaji huyo akisema hayo Nicodemus naye aliendelea kusisitiza kuwa eneo alilojenga Silvester lote alimuuzia.

“Hivyo kutokana na mkanganyiko huo nilichukua taarifa hizo na kumpelekea Katibu Tawala wa Wilaya Kilosa (DAS) ambapo zinaendelea kufanyiwa kazi”. Alimaliza kusema Afisa Mtendaji wa kijiji hicho.

Kufuatia sakata hilo mwanahabari wetu alimtafuta Silvester ambapo alipofika nyumbani kwake aliambiwa amesafiri kuelekea masomoni na alipomtafuta kwa njia ya simu kila alipompigia simu yake haikuwa hewani.

Leave a Comment