
MGOMBEA wa upinzani nchini Uganda katika nafasi ya urais, Bobi Wine, leo Januari 15, 2021, amepinga matokeo ya uchaguzi ambayo yametangazwa hadi sasa na kujitaja binafsi kama rais mteule, licha ya tume ya uchaguzi kusema kuwa siyo kura zote zilizokwishahesabiwa.
Bobi Wine anadai uchaguzi wa Alhamisi ulitawaliwa na wizi mbaya zaidi wa kura kuwahi kushuhudiwa katika historia ya Uganda, lakini hakutoa ushahidi wowote kuhusu madai yake.
Ametangaza kuwa mapambano ndiyo kwanza yameanza.
Mgombea huyo jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi, anasema kuwa atazungumza na waandishi wa habari saa chache zijazo juu ya kitakachofuatia.
Matokeo ya awali yanayotolewa na Tume ya Uchaguzi yanaonyesha Rais Yoweri Museveni anaongoza kwa zaidi ya asilimia 60.
Wakati huohuo, wanajeshi wameizingira nyumba ya Bobi Wine.