
PERFECT Chikwende tayari amesaini mkataba wa miaka miwili Simba akitokea FC Platinum ya Zimbabwe lakini taarifa ikufikie kuwa jamaa amekomba mil 127 hadi kukamilisha dili hilo.
Simba ilifanya umafia kwa kumteka Chikwende pale Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar, pia alikuwa anatakiwa na Azam FC ambao walizidiwa dakika za mwisho baada ya kuweka mezani mkwanja kiduchu.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo Championi Jumamosi linazo ni kuwa, kiungo huyo amekubali kujiunga na Simba kwa dau la dola 55,000 (Sh mil 126.8) alizowekewa mezani na mabosi wa Simba ambao waliamua kumteka uwanja wa ndege juzi usiku kufuatia Azam kumuwekea dola 50,000 (Sh mil 115.34) Championi linafahamu kuwa kiungo huyo alikuwa njiani kuja kujiunga na Azam ambao walipanga kumpokea saa saba ya mchana, juzi Alhamisi lakini uongozi wa Simba wakishirikiana na aliyekuwa kiungo wa zamani wa timu hiyo, Mzimbabwe, Justice Majabvi wakambadilishia ndege kiungo huyo badala ya kufika saa saba mchana akatua juzi saa moja usiku.

Licha ya uongozi wa FC Platinum na meneja wa kiungo huyo kuitambua Azam kama timu iliyopeleka ofa ya kumtaka kiungo huyo lakini Simba waliibuka kusikojulikana na kufanya umafia wa kumpora kiungo huyo akiwa njiani kuelekea kujiunga na Azam.

Baada ya kumpokea kiungo huyo walihakikisha wanamalizana naye kila kitu mapema kabla ya usajili kufungwa usiku wa kuamkia leo ambapo kwa sasa kinachosubiriwa ni kumtambulisha kiungo hiyo baada ya kumpa mkataba wa miaka miwili kwa dau hilo la Sh milioni 127.
“Chikwende yupo Dar na ameshamalizana na Simba ingawa safari yake ilikuwa ya kwenda Azam kabla ya uongozi wa Azam kukanusha kufuatia kocha George Lwandamina kuupinga usajili wake lakini ukweli Simba waliwazidi ujanja na kunasa saini ya kiungo huyo ambaye tayari yupo jijini akisubiria kutambulishwa tu,” alisema mtoa taarifa.
Stori: Ibrahim Mussa na Wilbert Molandi, Dar