×

Kocha Mbelgiji: Nipeni Simba Muone Mambo

IVAN Jacky Minnaert raia wa Ubelgiji ni mmoja kati ya makocha waliofanya mazungumzo na uongozi wa Simba kwa ajili ya kuchukua mikoba ya Sven Vandenbroeck raia wa Ubelgiji.

 

Simba ipo katika mchakato mzito wa kuhakikisha wanapata kocha mwenye rekodi kubwa kwa lengo la kufanya vizuri katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuondoka kwa aliyekuwa kocha wao.

 

Tayari majina ya makocha Rene Weiler raia wa Uswisi ambaye ni kocha wa zamani wa Al Ahly, Frolent Ibenge wa DR Congo na Hicham Aboucheroune wamekuwa wakihusishwa na kuwepo katika mpango lakini suala la mishahara yao mikubwa imekuwa kikwazo cha timu hiyo.

 

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya Bodi ya Wakurugenzi wa Simba zinadai kuwa uongozi wa timu hiyo umefanya mazungumzo ya siri na Mbelgiji huyo kwa lengo la kutaka kumpa kazi ya kuionoa timu hiyo.

Ipo hivi, uongozi wa Simba umekubaliana kutafuta kocha wa kawaida lakini ambaye wanaamini atakuwa na uwezo mkubwa katika timu hiyo ambapo wamefikia kufanya mazun-gumzo na kocha huyo anayeifundisha Al-Ittihad Tripoly inayoshiriki Ligi ya Libya.

 

Licha ya jambo hilo kufanyika kwa usiri mkubwa lakini Championi linafahamu kuwa Simba wamekuwa wakizungumza na kocha huyo kupitia mmoja wa mawakala wakubwa wa wachezaji mwenye asili ya Rwanda.

 

“Wamefanya mazungumzo na Ivan lakini bado hawajafikia pazuri kwa sababu wamemueleza wanataka kupata kocha mwenye uwezo mkubwa lakini siyo CV kubwa kama ilivyokuwa kwa Sven aliyeondoka ingawa bado wanaongea,” alisema mtoa taarifa.

 

Ivan Minnaert ni nani?Minnaert ni kocha wa Ubelgiji mwenye leseni ya Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA Pro) iliyotolewa mwaka 2012 na Chama cha Soka cha Hispania.

 

Kocha huyo amewahi kui-fundi-sha Djoliba AC ya Mali mwaka 2014 kabla ya mwaka 2016 kujiunga na AFC Leopards ya Kenya kisha mwaka 2017 alijiunga AS Kaloum Star ya Guinea akichukua mikoba ya Adda Benamar.

 

Lakini mwishoni mwa mwaka 2017 aliitwa katika kikosi cha Black Leopards ya Afrika Kusini katika nafasi ya usaidizi chini ya Jean-François Losciuto kabla ya mwaka huo kuchukuliwa na Mukura Victory ya Rwanda kwa mkataba wa miezi sita na baadaye akajiunga Rayon Sports ya Rwanda.

 

Mafanikio CAFKocha huyo akiwa na Rayon Sports, alifanikiwa kuipeleka katika Hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho kutoka katika kundi moja na Yanga, USM Alger na Gor Mahia ya Kenya.

 

Yanga wanamkumbuka kocha huyo baada ya kukubali kichapo cha bao 1-0 katika mchezo wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho mwaka 2018 baada ya kutoka sare katika mechi ya kwanza iliyopigwa jijini Dar.

Leave a Comment