
RAIS John Magufuli amewasili Mkoani Kagera na leo amezindua Shule ya Sekondari Ihungo ambayo imejengwa upya baada ya kuharibiwa na tetemeko la ardhi lililotokea 2016 pia ameweka jiwe la msingi la Chuo cha Veta-Kagera.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, amesema shule ya Ihungo iliyopo manispaa wa Bukoba mkoani Kagera sasa ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,152 kutoka idadi ya wanafunzi 640 iliyokuwa ikipokea kabla ya kujengwa upya.

Shule hiyo ilibomolewa na tetemeko la ardhi mwaka 2016, ndipo serikali ikachukua jukumu la kuikarabati na kuijenga upya ikiwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi wengi zaidi pamoja na mazingira mazuri ya kujifunzia.
Ndalichako amesema ujenzi wa shule hiyo umehusisha majengo ya madarasa na nyumba 30 za walimu ambazo zitawawezesha kufanya kazi karibu na shule.

Amesema ujenzi huo umehusisha pia ujenzi wa maabara za biolojia, kemia na fizikia, wameboresha mifumo ya maji na wameahidi kujenga barabara kipande cha kilomita moja kwa kiwango cha lami.