×

Matapeli Wamuibua Fiston Yanga, awatukana

MSHAMBULIAJI mpya wa Yanga, Fiston Abdul Razak, raia wa Burundi, ameibuka na kusema kuwa haijui Kampuni ya Uwakala ya Heritage Soccer Agency kwa kuwa hajawahi kufanya nayo kazi, hivyo wanachokifanya ni kitendo cha kitapeli.

 

Katikati ya wiki hii ilisambaa barua iliyokuwa imeambatanishwa katika Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Shirikisho la Soka Afrika (Caf) na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ikidai mshambuliaji huyo amekiuka mkataba na kusaini Yanga bila ridhaa yao kama wasimamizi wake.

 

Mshambuliaji huyo ameliambia Championi Jumatatu kuwa hawatambui watu hao wanaodai hivyo huku akiamini ni matepeli kwa kuwa hajawahi kufanya nao kazi yoyote licha ya kuiona barua iliyoandikwa ikionyesha malalamiko hayo.

 

“Hao jamaa ni matapeli na hiyo barua nimeiona, nikawapigia simu, nikawatukana na nimewaambia huo mnaofanya ni utapeli na kama wanawafanyia wachezaji wengine huko watakuwa hawawatendei haki hata kidogo.

 

“Huwa sipendi ujinga na kitu wanachokifanya siyo kabisa kwa sababu sijawahi kufanya nao kazi, hawajawahi kunipa dili yoyote, hata ya majaribio, kwa nini waseme hivyo na ukiangalia hiyo barua yao imekatwa kwa chini, nafanya kazi na wakala watatu ambao ni raia wa Misri ila siyo wao maana hao wanaodai hivyo mmoja ni Mtanzania na tulishagombana,” alisema Fiston.

Leave a Comment