
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ameshiriki mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Manyara, Martha Umbulla, na ametumia fursa hiyo kuwasihi wananchi wamuenzi kwa kuayaendeleza mambo mema aliyofanya katika kipindi cha uhai wake.
Mazishi hayo ya Martha yamefanyika jana (Jumanne, Januari 26, 2021) nyumbani kwake katika kijiji cha Dongobesh wilayani Mbulu Mkoa wa Manyara. Mbungea huyo alifariki Jumanne, Januari 21, 2021 katika Hospitali ya HCG Mumbai, India alikokuwa anatibiwa.
“Nimekuja kuungana nanyi kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, kutoa pole kwa mume wa marehemu, watoto na familia kufuatia msiba mzito wa kuondokewa na mpendwa wetu Mheshimiwa Umbulla,” alisema.

Kwa upande wake, Naibu Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson akizungumza kwa niaba ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, amesema Bunge limempoteza mtu muhimu sana na litamkumbuka marehemu Martha kwa mchango mkubwa alioutoa enzi za uhai wake. Amesema marehemu Martha alikuwa mlezi kwa wabunge wapya wanaoingia bungeni.

Naye, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul akizungumza kwa niaba ya wabunge wa mkoa wa Manyara amesema marehemu amewafundisha mambo mengi ikiwemo kufanya kazi kwa bidii, upendo, uvumilivu, kusamehe na kuomba msamaha pamoja na kumcha Mwenyezi Mungu.
Awali, akisoma wasifu wa marehemu mtoto wa kwanza wa marehemu, Innocent Umbulla, alisema Martha Umbulla alizaliwa Novemba 10, 1955 katika kijiji cha Dongobesh wilayani Mbulu na alikuwa mtoto wa mwisho katika familia ya watoto wanne.
Alisema mwaka 1963 hadi 1969 alipata elimu ya msingi katika shule ya msingi Dongobesh na baadaye aliendelea na masomo ya sekondari katika shule ya wasichana ya Korogwe mwaka 1970 hadi 1973. Mwaka 1974 hadi 1975 alisoma shule ya sekondari ya wasichana ya Tabora.
“Mwaka 1976 alihudhuria kwa mujibu wa sheria mafunzo Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kambi ya Ruvu na mwaka 1977 hadi 1979 alisoma stashahada ya kilimo katika Taasisi ya Kilimo Ukiliguru Mwanza. Mwaka 1989 hadi 1990 alisoma shahada ya juu katika chuo cha Reading , Uingereza na mwaka 2000 hadi 2002 alisoma shahada ya uzamili katika fani ya usimamizi wa biashara nchini Netherland.

Ibada ya mazishi ilifanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mbulu Jimbo la Dongobesh na kuongozwa na Msaidizi wa Askofu wa Jimbo la Mbulu Mchungaji John Nade ambaye aliwasisitiza waombolezaji wajiandae kukutana na Mwenyezi Mungu kwa sababu hawajui siku wala saa.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU.