
ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Ufunuo lililopo Kimara Bonyokwa jijini Dar es Salaam, Mchungaji Paul Bendera, amewakosoa wanaojiita watumishi wa Mungu ambao wamekuwa wakidai kuwa makanisa yanayotumia mafuta kama njia mojawapo ya upako wanatumia mafuta ya binadamu.
Askofu Bendera amesema hayo wakati wa mahubiri yake katika Ibada ya Jumapili, Januari 17, 2021, kanisani hapo na kuongeza kuwa watu wanaotoa kauli hizo wameishiwa maneno, wamekosa busara na hekima na wana nia ovu na kanisa la Mungu kwani hakuna kanisa ambalo linaweza kutumia mafuta ya binadamu.
“Vita ya kidini haijaanza leo, watu kama hawa msiwasikilize, ni wapotoshaji na wanataka kuwatia hofu waumini. Hivi una akili timamu unasimama na kusema nilikuwa nagawa mafuta ya binadamu, na hapa bado nina chupa ya mafupa, basi tuonyeshe hicho kiwanda cha kukamulia hayo mafuta kipo wapi? Usitukane watu wakati huna akili.
“Unasema makanisa yanayokuwa ni freemason, hebu tuambie hizo ofisi zao ziko wapi, wanaotoa watu wafe? Hii ni kuwaogopesha watu, mtu anajipaka mafuta mpaka nyumbani wewe utawazuiaje? Hawa wapuuzi kinachowasumbua wamepokea uamsho kutoka Ulaya, dini zao zimetoka Ulaya kana kwamba sisi huku Mungu hayupo au hawezi kuinua watu,” amesema Askofu Bendera.