
IKIWA ni siku moja tu tangu Rais John Magufuli kutaka Wizara ya Afya kutokimbilia chanjo ya corona, Shirika la Afya Duniani (WHO) limeitaka Tanzania kujiandaa kupokea chanjo ya corona kama mataifa mengine duniani.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kwa njia ya mtandao, Mkuu wa WHO Kanda ya Afrika, Dkt. Matshdiso Moeti amesema Tanzania inatakiwa kutumia mwanya wa upatikanaji wa chanjo kwa faida ya wananchi na Kanda ya Afrika Mashariki kwa jumla.
”Tumeanza kuwasiliana upya na ngazi za juu za uongozi, na tunatoa mchango wetu kama ilivyokuwa hapo mwanzo, na tunataka kushirikiana na Tanzania, kwa niaba ya watu wa Tanzania, nchi jirani na dunia kwa ujumla. Sehemu ya mawasiliano yetu na Tanzania ni kukumbusha serikali kuwa hii ni sehemu ya makubaliano ya kanuni za afya za kimataifa ambapo nchi wanachama wamekubali kwa pamoja kuzuia kusambaa kwa magonjwa,” amesema Moeti.
WHO inasema kuwa imekuwa ikitoa mchango na kuwasiliana na serikali ya Tanzania kuanzia mwanzo wa janga hili la corona. Shirika hilo pia limesisitiza Tanzania kutoa takwimu za mwenendo wa corona nchini humo ili iwe rahisi katika kupambana na kuzuia maambukizi mapya.
Naye Katibu Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, Tedros Ghebreyesus, anasema anaunga mkono alichosema @MoetiTshidi, anatoa rai hatua dhabiti za kiafya kukabiliana dhidi ya corona zinapaswa kufuatwa na kujiandaa kupokea chanjo.
Takwimu ni suala muhimu pia kwa Tanzania kuzitoa, hasa baada ya matukio miongoni mwa wasafiri na wageni katika miezi ya hivi karibuni. Hatua hii ya WHO inakuja siku moja baada ya Rais wa Tanzania, John Magufuli, kutahadharisha kuhusu chanjo ya Covid-19 ambayo imeanza kutolewa katika mataifa mbalimbali duniani.
Alipozungumza katika uzinduzi wa shamba la miti huko wilayani Chato mkoani Geita, alizungumzia pia kuhusu hali ya corona nchini na kuwasihi wananchi kuendela kuomba pamoja na kujifukiza.
”Tutaendelea kuchukua tahadhari, pamoja na kujifukiza, kusali na kuswali, huku tukiendelea na shughuli zetu; ule vizuri ushibe ili corona ashindwe kuingia kwenye mwili wako,” alisema.
Aidha kuhusu uwepo wa aina mpya ya corona, Magufuli alisema kuwa kuna baadhi ya Watanzania walienda kupata chanjo huko nje lakini wakaleta aina mpya ya corona. ‘
‘Ninajua kuna baadhi ya Watanzania hata wameondoka ndani ya nchi na kukimbilia maeneo mengine na kwenda kuchanjwa na walivyochanjwa wakaja huku wakatuletea corona ya ajabu-ajabu,” alisema Magufuli.
Pia alisisitiza juu ya madhara ya chanjo, hususani kuwa hakuna chanjo za magonjwa sugu ya muda mrefu kama ukimwi saratani.
‘Tusiwe tunakimbilia masuala ya chanjo-chanjo, si kila chanjo ina faida kwetu, ni lazima Watanzania tuwe macho, tuwe waangalifu, tutafanyiwa majaribio, tuendelee kumuomba Mungu wetu na tuendelee kuchukua tahadhari,” alisisitiza.
CHANZO: BBC SWAHILI