
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amewataka wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kote nchini kuhakikisha wanakaa vikao vya kamati za maadili na kutatua changamoto za kimaadili kwa baadhi ya watumishi.
Magufuli ametoa uamuzi huo leo Jumatatu, Februari 1, 2020, wakati akitoa hotuba yake wakati wa hafla ya maadhimisho ya miaka 100 ya Mahakama Kuu ya Tanzania.
“Nimesikia kamati za maadili za maofisa wa mahakama za mikoa na wilaya hazikutani, wamepewa hayo madaraka Ma-RC, Ma-DC kwa ajili ya kushughulikia masuala ya maadili hawakutani na hivyo kushindwa kuchukua hatua za kinidhamu kwa watumishi wenye makosa.
“Nawaagiza Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wote kuhakikisha Kamati za Maadili zinakutana, mwezi huu wa pili nataka nipate ripoti wamekutana mara ngapi, unaweza kulaumu huku kumbe waliopewa madaraka ya kusimamia wamekaa kimya.
“Kuna tabia ya baadhi ya wateja wa Bank kukimbilia Mahakamani na kufungua kesi nyingi au kuweka mazuio ili kuchelewesha urejeshaji wa mikopo wanayodaiwa, kesi hizo zipo nyingi na nyingine zina hadi miaka mitano hazijatolewa maamuzi, inaleta athari kwa Bank.
“Mahakama ishughulikie kwa haraka kesi kama hizi za (wanaofungua kesi ili kuchelewesha marejesho ya mikopo), ili zisiathiri uchumi wa nchi yetu, kuna Wafanyabiashara kazi yao ni kwenda kuzipark kesi wanaita parking, hii inaziumiza Taasisi za Kifedha.
“Wapo baadhi ya watu wanaodai kuwa tangu tumepata Uhuru hakuna chochote kilichofanyika, hawajui wakati tukipata Uhuru kulikuwa na majengo 4 tu ya Mahakama Kuu, hapakuwa na Jaji yoyote Mtanzania, barabara za lami zilikuwa KM 300, sasa zinakaribia kufikia KM 15,000.”
“Hawajui kuwa wakati tunapata uhuru tulikuwa na majengo manne tu ya Mahakama Kuu na hapakuwa na Jaji yoyote Mtanzania mpaka mwaka 1960, ndipo Majaji wawili wa kwanza waliteuliwa na wote walikuwa wanaume, Jaji wa kwanza mwanamke aliteuliwa 1973.