
WATU wanne wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kwa mashtaka mawili likiwemo la kukutwa na nyara za Serikali zenye thamani ya sh. mil 45.9.
Washtakiwa hao ni Idd Selemani (47), Maria Mole (29), Abubakar Sauka (50) na Hassan Salum (56) ambapo wamefikishwa mahakamani hapo wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 6 ya mwaka 2021 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba na kusomewa mashtaka yao na Wakili wa Serikali, Candid Nasua.

Wakili Nasua amedai kuwa washitakiwa hao, mnamo Januari 13, 2021, wakiwa eneo la Magomeni Mwembechai, Wilaya ya Kinondoni Dar es Salaam, washitakiwa walikutwa na meno tisa ya simba yenye thamani ya Dola za Marekani 2309.83 sawa na Tsh. 11,318,167 mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Katika shtaka la pili, washtakiwa wanatuhumiwa siku hiyo na mahali hapo walikutwa na vipande 32 vya bidhaa ambavyo vimetengenezwa na meno ya tembo vyenye thamani ya Dola za Marekani 15,000 sawa na Sh. 34,647,450 mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo Hakimu Simba amewaeleza kuwa hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi.
Nasua amedai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika, ambapo kesi imeahirishwa hadi Februari 16, 2021, itakapotajwa na washitakiwa hao wamerudishwa rumande.