×

Majaliwa: Halmashauri Zikamilishe Madarasa kwa Mapato Yao

 

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ameagiza halmashauri zote nchini kutenga bajeti kwa kutumia mapato yao ya ndani kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa ulioanzishwa na wananchi kwa lengo la kuwezesha wanafunzi wa kidato cha kwanza kuanza masomo.

 

 

Majaliwa ametoa kauli hiyo leo, Alhamisi Februari 4, 2021, katika kipindi cha maswali ya papo kwa hapo wakati akijibu swali la mbunge wa Sengerema (CCM), Hussein Tabasamu.

 

 

Mbunge huyo alihoji kuhusu Serikali kutoa fedha kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa vyumba vya madarasa ili wanafunzi wote wa kidato cha kwanza kuhakikisha wanakuwa darasani ifikapo Februari 28, 2021.

 

 

Desemba, 2020 Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo, alisema wanafunzi 74,166 sawa na asilimia 8.9 ambapo wavulana ni 34,861 na wasichana 39,305 hawakupangiwa shule katika awamu ya kwanza kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa.

 

 

“Ni kweli halmashauri zimekuwa na utamaduni wa kushughulikia majengo hayo kwa dharura kila mwaka, lakini sasa tumeagiza halmashauri wawe na mpango wa kudumu kwa kutumia takwimu tulizonazo.

 

 

“Halmashauri zote zinafahamu kila mwaka zina wanafunzi wangapi wanaotaka kumaliza mwaka huo na ambao wanaweza kufaulu. Upo utaratibu wa kuwafahamu; jambo hili linakwenda sambamba na agizo nililotoa, lakini tumekuta tayari maboma mengi yamejengwa na wananchi na hayajakamilika,” amesema.

 

 

Amesisitiza kwamba pamoja na kutenga mapato yao, Tamisemi imekuwa ikitenga bajeti kwa ajili ya kuunga mkono ukamilishaji wa majengo yaliyoanzishwa na wananchi licha ya uhaba wa bajeti hiyo.

 

Leave a Comment