×

Fiston Afungua Akaunti ya Mabao Yanga

AKICHEZA mchezo wake wa kwanza, mshambuliaji mpya wa Yanga Mrundi Fiston Abdoul Razack amefungua akaunti ya mabao baada ya kupiga hat trick katika ushindi wa mabao 4-2 walioupata timu hiyo.

 

Hiyo ni baada ya kujiunga na timu hiyo wiki iliyopita akisaini mkataba wa miezi sita kama mchezaji huru katika usajili wa dirisha dogo lililofungwa Januari 15, mwaka huu.

 

Yanga imemsajili mshambuliaji huyo kwa ajili ya kuiboresha safu ya ushambuliaji ya timu hiyo inayoongozwa na Mrundi mwenzake Said Ntibazonkiza ‘Saido’, Michael Sarpong, Yacouba Songne na Ditram Nchimbi.

Mshambuliaji huyo alipiga hat trick hiyo katika mchezo wa kwanza wa kirafiki waliocheza dhidi ya timu yao ya vijana ya U20 uliopigwa juzi jioni kwenye Uwanja wa Avic Town, Kimbiji, Kigamboni jijini Dar ambako ni sehemu ambayo Yanga imeweka kambi.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumamosi, mshambuliaji huyo alifunga mabao hayo matatu pekee huku moja likifungwa na Waziri Junior aliyepishwa na Fiston katika kipindi cha pili.“Kocha ameomba mechi mbili za kirafiki kabla ya kuanza ligi iliyosimama na lengo ni kutengeneza mechi fitinesi na muunganiko wa timu.

 

“Hivyo alianza kwa mchezo huo wa kirafiki dhidi ya U20 na mchezo mwingine tutacheza na African Sports keshokutwa (kesho) Jumamosi saa moja usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex, Mbagala.“Katika mchezo huo, kocha atamuanzisha Fiston kucheza pamoja kati ya Niyonzima (Haruna) au Carlinhos (Carlos Ferandez) watakaocheza nyumba yao namba 10 huku yeye 9,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Akizungumzia mchezo dhidi ya African Sports, Kaze alisema kuwa: “Tulitarajia kuwa na mechi zaidi ya mbili za kirafiki, lakini kutokana na ratiba na muda wa timu nyingi kwa hivi sasa, tumepata hizo mbili na moja tayari tulicheza na timu yetu ya vijana ya U20 na nyingine tutacheza dhidi ya African Sports. “

 

Kuna baadhi ya upungufu ambao nazidi kuufanyia kazi kwa vijana wangu, nina imani kubwa na kikosi changu kufanya vizuri katika michezo ijayo kwa kuanzia na mchezo wetu wa ligi dhidi ya Mbeya City.

Stori: Wilbert Molandi, Dar es Salaam | Chapioni Jumamosi

Leave a Comment