
POLISI katika kaunti ya Nyandarua nchini Kenya wanachunguza hali iliyosababisha kifo cha mzee mmoja mwenye miaka 58, ambaye ameaga dunia akifanya mapenzi.
Kulingana na ripoti ya polisi, Edith Wairimu Mwangi (55), alimkuta marehemu akihema sana baada ya kwenda kusafisha chumba hicho katika nyumba ya kulala wageni ya Heshima Lodge Olkalau.
Kufuatia hali hiyo mwanamke huyo alikimbia katika Kituo cha Polisi cha Olkalau kutoa ripoti ambapo maafisa wa polisi walifika eneo la tukio wakiandamana na makachero kutoka Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI).
Ambulensi ilitafutwa na alikimbizwa katika Hospitali ya JM Kariuki ambapo alithibitishwa kufariki dunia.
“Wakati mwili wake ulikuwa unakaguliwa, alipatikana na kondomu kwenye uume wake. Eneo la tukio lilichunguzwa na maafisa wa CSI kabla ya mwili huo kupelekwa mochari ukisubiri kufanyiwa upasuaji,” ilisoma ripoti ya polisi.
Mwanamme huyo pia alikuwa mlinzi wa Lodge hiyo na bado haijajulikana alikuwa na mwanamke yupi. Kisa hiki kinakuja siku chache baada ya mwanamme mwingine mwenye miaka 52, kuzirai na kufariki usiku wa Jumatano, Februari 3.
Wiki mbili zilizopita tuliripoti kisa kingine ambapo mzee mwenye umri wa miaka 80 aliaga dunia katika njia isiyoeleweka akijivinjari na mrembo wa miaka 33 katika hoteli moja Dar es Salaam, Tanzania.
David Mluli alipatikana ameaga dunia Jumamosi, Januari 16 katika chumba nambari 22 Mbezi Garden ambapo alikuwa ameenda kustarehe na mrembo Neema Kibaya ambaye alikamatwa kutokana na kisa hicho.
Chanzo – Tuko News