
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt Dorothy Gwajima, ameagiza kusimamishwa kazi Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Chunya, Dkt Felista Kisandu, kwa kukiuka mwongozo wa utoaji wa taarifa za milipuko ya magonjwa kama ilivyoelezwa kwenye Sheria ya Afya ya Umma (Public Health Act) ya mwaka 2009.
Akitoa tamko hilo jana Jumapili Februari 7, 2020, Gwajima amesema Kisandu anapisha uchunguzi kufuatia sakata la kusambaa kwa taarifa ya mlipuko wa ugonjwa usiofahamika katika kata ya Ifumbo wilayani Chunya.
“Kutokana na kadhia hii ambayo imeleta taharuki isiyo ya lazima naiagiza mamlaka ya ajira ya Dk Felista Kisandu ambaye ni Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Chunya ichukue hatua za kumsimamisha kazi ili kupisha uchunguzi chini ya Baraza la Madaktari na taarifa nipate ndani ya siku kumi,” amesema Gwajima.
Ameongeza kwamba katika Kata ya Ifumbo, Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya, hakuna mlipuko wa ugonjwa wowote uliothibitishwa wala hakuna janga lolote la kiafya kama ilivyoripotiwa na vyombo vya habari.
Amesisitiza kwamba timu ya wataalamu imefanya mahojiano na wananchi na kubaini hakuna vifo 15 kwa mara moja vya wagonjwa wanaodaiwa kuwa na dalili za kutapika damu kama ilivyoripotiwa na diwani wa Kata ya Ifumbo na takwimu hizo hazijawahi kuripotiwa popote.