
SADIKIELY META (71) mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya kufanya biashara haramu ya kusafirisha binadamu, (kutumikisha walemavu) kukwepa kodi na kuisababishia hasara Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kiasi cha T sh. milioni 31 amefariki dunia katika Hospitali ya Temeke alikokuwa akipatiwa matibabu.
Meta na wenzake 14 alikuwa akikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 2 ya mwaka 2021 yenye mashtaka 41 yakiwemo ya kusafirisha na kutumikisha walemavu kwa kuwafanya kuwa kuomba barabarani.
Akitoa taarifa juu ya kifo cha mshtakiwa huyo wakili wa utetezi, Robert Langeni ameeleza hayo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Februari 9, 2021, mbele ya hakimu mkazi mkuu, Kassian Matembele.
Wakili huyo amesema Meta aliugua akiwa gerezani na kupelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Temeke kwa matibabu lakini Januari 28, 2021 alifariki dunia.
Aliieleza mahakama kuwa Meta alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa kisukari na tayari mazishi yalishafanyika wiki iliyopita mkoani Moshi, Kilimanjaro.
Wakili wa Serikali, Kija Luzungana, ameieleza mahakama hiyo kuwa kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi bado haujakamilika.
Hakimu Matembele baada ya kusikiliza hoja za pande zote ameaihirisha kesi hiyo hadi Februari 23, mwaka huu, itakapotajwa. Kesi hiyo imeendeshwa kwa mfumo wa digitali yaani njia ya video ambapo kesi hiyo ina jumla ya washtakiwa 14 ambao wote wapo Segerea.