
MBUNGE wa kuteuliwa, Humphrey Polepole, leo Jumanne Februari 9, 2021 amelieleza Bunge kuwa Rais wa Tanzania, John Magufuli hana mpango wa kuongeza muda wa kukaa madarakani.
Hata hivyo, amesema hawezi kuzuia mijadala ya wabunge kwa kuwa ni haki yao kusema kile wanachokiamini ndani ya Bunge.
Polepole ambaye ni katibu wa itikadi na uenezi wa CCM amesema ndani ya chama chao walishaelezwa hivyo na itabaki hivyo bila kubadilika.
Ametoa taarifa hiyo leo baada ya kuomba taarifa kufuatia kauli ya mbunge wa Konde (ACT-Wazalendo), Khatibu Said Haji kumtaja Polepole kwamba alitumwa na Rais kusema juu ya kutogombea lakini amekaa kimya.
Khatibu amesema kitendo cha kukaa kimya kinawafanya wabunge kuendelea kumtaka Rais Magufuli avunje Katiba wakati aliapa kuilinda.
“Nampongeza Rais Magufuli kwa uamuzi wake wa kuiheshimu katiba ya nchi hii, kabla yetu alitangulia kuapa, uamuzi wake wa kumtuma Polepole awaambie wana CCM kwamba hataongeza kipindi cha utawala ni ishara kwa kiongozi wetu kuilinda katiba.
“Mheshimiwa Polepole waambie CCM, Mheshimiwa Rais Magufuli hana shida ya kuongeza muda, alikutuma na video zinatembea tunaziona kwa nini unawaacha akina Sanga hapa wanaendelea kupotosha? Kwa nini hamheshimu mawazo ya Mheshimiwa rais?
“Bunge lililopita nilimwambia Ally Keissy, alinyanyuka na kujipendekeza hivihivi nyenyenyeee! Nikamuambia nchi hii ni ya kidemokrasia na rais anaheshimu katiba na ameshasema hataongeza muda kama mna wasiwasi hamna mtu wa kutoa rais sisi wapinzani tunao,” amesema Khatibu Haji.
“Naomba kumpa taarifa mbunge kwamba masuala ya CCM yanazungumziwa kwenye vikao vya chama, hapa Bungeni wabunge wana uhuru wa kuzungumza lakini kinachozungumzwa hapa ndani hakiathiri msimamo wa chama tumekwishautoa rais hataongeza muda. Sisi ndani ya chama tulishaelezana na yeye (rais) ndiyo msemaji mkuu, lakini humu bungeni haizuii wao kutoa maoni yao,” amesema Polepole.
Katika michango ya wabunge, Deo Sanga (Makambako) na Joseph Msukuma (Geita Vijijini) waliibua hoja iliyoanzia Bunge la 11 wakimtaka Rais Magufuli kufikiria namna ya kuongeza muda wa kuwa madarakani.