
ULE utajiri uliotengeneza vichwa vya habari wa video vixen na msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Irene Louis ‘Lyyn’, unadaiwa kuyeyuka, RISASI limedokezwa.
Lyyn ambaye aliwahi kugandwa na skendo ya kutoka kimapenzi na Bosi wa Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, anadaiwa kuwa juu ya mawe kwa sasa.
Lyyn amekuwa akionekana akila bata kupita maelezo huku akiishi kwenye majumba ya kifahari ya ghoroga maeneo ya ushuani na kutembelea ndinga kali zaidi ya moja ambazo amekuwa akidai kwamba ni mali zake, lakini sasa mambo yamegeuka.

Ubuyu wa mtoto unadai kwamba, Lyyn amecharara kiasi cha kuamua kuuza baadhi ya magari yake likiwemo moja aina ya Toyota Mark X alilokuwa akivimba nalo mtaani.
Kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika, mrembo huyo anayetikisa na wimbo wake wa Maneno, amekuwa akipitia wakati mgumu kwa sababu hata mjengo wa kifahari aliyokuwa akiishi awali, amehama kwa sababu ya kukosa pesa za kulipia kodi.
“Yaani hapa ninavyokuambia, gari lake lipo kwenye yadi ya kuuzia magari, lipo sokoni linauzwa.“

Lile gari lake lingine aina ya Jeep liligongwa na limeharibika vibaya mno,” kinasema chanzo hicho ambacho ni mtu wa karibu wa Lyyn.Baada ya kujazwa ubuyu huo, Gazeti la RISASI lilimtafuta Lyyn ili kupata undani wa skendo hiyo ya kufulia ile mbaya ambapo alisema kila mtu ana maisha yake na si vyema mtu kumfuatilia kila anachofanya.
Anasema kwa ukali kuwa, kama gari anauza si ananunua lingine? Shida iko wapi?“Naomba mniache kabisa, nilinyamaza kwa sababi sipendi drama hata kidogo na isitoshe ni kwamba kuuza gari si ndiyo kununua lingine? “Watu waniache, waache kufuatilia maisha yangu,” anasema Lyyn na kuongeza;“Juhudi zangu ndizo zilizonifikisha hapa nilipo.”
Mbali na magari hayo mawili ya Toyota Mark X na Jeep, pia Lyyn alikuwa na magari mengine makali kama BMW, Jaguar na Volkswagen ambayo nayo haonekani akivimba nayo kama zamani.