
KOCHA Mkuu wa Yanga, Cedric Kaze amesema kuwa kuna watu ambao wanawakatisha tamaa kuelekea kwenye mbio za kusaka ubingwa wa Ligi Kuu Bara baada ya jana kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Mbeya City, Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Mchezo huo ambao ulitawaliwa na ubabe mwanzo mwisho, dakika 45 za kipindi cha kwanza zilikamilika kwa wababe hao wawili kushindwa kufungana.

Kipindi cha pili, Kaze alifanya mabadiliko kwa kumuingiza Deus Kaseke akichukua nafasi ya Farid Mussa, kuingia kwake aliweza kuongeza kasi ya ushambuliaji kwa Yanga, akafanikiwa kupachika bao dakika ya 84 bao ambalo lilileta utata kutokana na mchezaji wa Mbeya City kuonekana akiokoa mpira huo kabla ya kuzama ndani ya nyavu.
Baada ya kufungwa bao hilo, wachezaji wa Mbeya City walionekana kumlalamikia mwamuzi na iliwachukua dakika moja kurudi kwenye mchezo ambapo waliweza kufanya shambulizi lililozaa penalti dakika ya 90 baada ya Yassin Mustapha kunawa mpira ndani ya 18.

Penalti ya Mbeya City ilifungwa kiufundi na Pastory Athanas ambaye alimchambua mlinda mlango namba moja wa Yanga, Metacha Mnata.Baada ya mwamuzi kumaliza mchezo huo, wachezaji wa Yanga walionekana kumfuata wakimlalamikia huku Lamine Moro, nahodha wa kikosi hicho akiwatuliza wenzake.
Kaze alisema kuwa: “Kuna watu ambao wanatukatisha tamaa kwenye mbio zetu za ubingwa ila tunaamini kwamba tutafanya vizuri kwenye mechi zetu zijazo.

”Ingizo jipya la Yanga, Fiston Abdoul Razack lilitumia dakika 74 na nafasi yake ilichukuliwa na Ditram Nchimbi.Kwa matokeo hayo, Yanga imeendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara ikifikisha pointi 45
⚫️ Kwa UPDATES zote, Download GLOBAL APP: ⚫️ ANDROID:http://bit.ly/38Lluc8 ⚫️ iOS:https://apple.co/38HjiCx