×

Serikali Yasaka Tril 1.029 Kodi ya Ardhi Moro

 

OFISI ya Ardhi Mkoa wa Morogoro imeanza kuwabana wadaiwa wa kodi ya pango la ardhi kwa kuwafikisha wadaiwa sugu 50 wanaodaiwa kiasi cha shilingi 1.552,436,750 katika Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ikiwa ni mkakati wa ofisi hiyo kukusanya madeni na malimbikizo mengine ya ardhi yanayofikia trilioni 1.029.

 

 

Akizungumza ofisini kwake mwishoni mwa wiki mkoani Morogoro, Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa, Frank Mizikuntwe, alisema  wadaiwa waliofikishwa kwenye baraza hilo ni sehemu ya wadaiwa wa kodi ya ardhi 474 aliowaeleza kuwa kufikia tarehe 8 Machi 2021 mashauri yao yatakuwa yamesikilizwa katika baraza hilo.

 

 

Alisema, kati ya wadaiwa 50 ni wadaiwa 21 tu ndiyo waliojitokeza kusikiliza mashauri yao ambao, hata hivyo kwa kujibu wa Frank walikubali kulipa malimbikizo yao kwa awamu kufikia mwisho wa mwezi juni 2021.

 

 

Aliongeza kwa kusema kuwa, kwa wale wadaiwa wasiofika kusikiliza mashauri yao sambamba na watakaoshindwa kukamilisha madeni katika muda waliokubaliana ofisi yake itasubiri amri ya  baraza  kwa hatua zaidi ambapo maamuzi yake ni kunadiwa mali za wadaiwa kufidia deni.

 

 

Alisema, ofisi ya ardhi mkoa wa Morogoro katika kuwafuatilia wadaiwa sugu imeelekeza nguvu kubwa katika halmashauri zenye madeni makubwa ambapo alizitaja kuwa ni Manispaa ya Morogoro trilioni 1.006, Ifakara TC bilioni 11, Kilosa bilioni 6 pamoja na halmashauri ya wilaya ya Mvomero shilingi bilioni 3.8.

 

 

Na Munir Shemweta, WANMM MOROGORO

Leave a Comment