
SENETA wa Garissa, Mohamed Yusuf Haji amefariki, familia yake imethibitisha.
Haji ambaye hadi mwaka 2020 alihudumu kama Mwenyekiti wa Jopokazi la Maridhiano (BBI) alifariki katika hospitali ya Aga Khan, leo Jumatatu asubuhi baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Msemaji wa familia alisema Haji alifariki baada ya baadhi ya viungo vya mwili wake kufeli kufanya kazi. Kabla ya kulazwa hospitalini mwaka 2020 Seneta Haji aliripotiwa kupata jeraha la kiuno baada ya kuanguka nyumbani kwake.
Tangu wakati huo amekuwa akilazwa katika hospitali mbalimbali kwa matibabu. Alikuwa amerejea nchini Jumamosi wiki jana kutoka Uturuki ambako alipelekwa Desemba 2020 kwa matibabu zaidi.
Amefariki akiwa na umri wa miaka 80. Rais Uhuru Kenyatta ametuma salamu za pole akifariji familia ya Haji, marafiki na wakazi wa Kaunti ya Garissa.