
KOCHA Mkuu wa Yanga, Mrundi, Cedric Kaze amefunguka kuwa licha ya kupata matokeo ya sare katika mechi mbili mfululizo lakini bado anaamini wana nafasi ya kupigania ubingwa wa msimu huu kwa kuhakikisha wanapata matokeo katika mechi zao zijazo ikiwemo ya leo Jumamosi dhidi ya Mtibwa Sugar.
Yanga inatarajia kucheza na Mtibwa, leo Jumamosi katika mchezo unaotarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, saa moja usiku.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Kaze alisema kuwa wamekuwa wakipambana kuhakikisha wanashinda kila mchezo bila ya kujali wanakutana na ugumu gani katika mechi zao kwa kuwa malengo yao yapo kwenye kuwania ubingwa wa msimu huu.

“Tunajua ligi imekuwa ngumu lakini kila timu imekuwa ikijitoa kutafuta matokeo kwa kuwa ligi ipo katika mzunguko wa pili, hivyo kila mmoja anataka kuhakikisha anakuwa kwenye wakati mzuri, inatulazimu tubadili mipango yetu ili kuweza kufikia malengo.“
Presha imekuwa kubwa kwa sababu tunaongoza ligi lakini hali hii inatufanya kutambua wapi tumekuwa tukikosea kwa kuhakikisha tunapata matokeo mazuri katika kila mchezo kuanzia kwenye mchezo wetu wa Jumamosi (leo) ili kuweka malengo yetu katika wakati mzuri,” alisema Kaze.
Mchezo wa mwisho baina ya timu hizi uliopigwa Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro Yanga ilishinda bao 1-0. Kwa sasa Yanga wako kileleni wakiwa na alama 46 na Mtibwa wako nafasi ya 11 na alama zao 23.
Stori na brahim Mussa, Dar es Salaam