
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewashukuru viongozi wa dini kwa kuendelea na maombi ya siku tatu.
Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Jumamosi, Februari 20, 2021, wakati wa ibada ya kumuaga aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi ikiendelea katika Kanisa Katoliki Jimbo la Tanga Parokia ya Mt. Augustino Manundu Korogwe.
Majaliwa ambaye amewaongoza waombolezaji katika mazishi hayo Kitaifa amesema serikali inawapenda wananchi wake na inaendelea kufuatilia magonjwa mbalimbali nchini, hivyo wananchi waendelee kuchukua tahadhari huku akiwasihi kujiridhisha na barakoa wanazovaa na ikiwezekana wavae barakoa za kutengeneza wenyewe hapa nchini.
“Barakoa hizi ni bora tukajiridhisha zinatoka wapi, bora ukatengeneza ya kwako au iliyotengenezwa hapa nchini Tanzania, barakoa ni kinguo tu kinachozuia hayo mate yasije yakatoka au ukapokea vitu vingine hili jambo ni muhimu sana tulizingatie.
“Tuna Rais wetu makini sana ameendelea kutuongoza vizuri ametusihi tuondoe hofu, lakini muhimu ndani tunaendelea kupambana kuhakikisha kwamba usalama wa watu wetu nchini unaendelea kuwepo barakoa hizo mnazozivaa tulisema ni bora tukajiridhisha.
“Hata Mh Rais jana alivyokuwa anaeleza umma wa Watanzania kuondoa hofu, aliwaomba viongozi wa dini kutuongoza kufunga siku tatu na kuendelea na maombi naomba nitumie nafasi hii kuwashukuru sana viongozi wa dini.
“Nimeshuhudia jana Swala zote za Ijumaa wameanza kutekeleza kwa kuzungumza na waumini kuliombea Taifa, Wasabato nawashukuru sana wanaendelea kuliombea Taifa, hata Baba Askofu pia anamaandalizi ya wakatoliki kesho kuendelea kuliombea Taifa hili.
“Niwasihi Watanzania wakati huu Dunia ikiwa kwenye mahangaiko ya magonwa ya maambukizi sisi tuwe watulivu, serikali yenu inawapenda tumejikita kuhakikisha tunafuatilia na kuona mwenendo wa magonjwa haya, tuna magonjwa mengi tuna Malaria, UKIMWI.
“Tuna BP, Sukari na magonjwa chungu nzima, wataalamu wetu huko kwenye mahospitali walio kwenye maabara wanaendelea kuchunguza na kujikita katika kutoa huduma na Mh Rais ametusihi kwamba kipindi hiki sote tuendelee kuzingatia masharti ya afya.
“Nimeona leo tabia ambayo tuliizungumza hata mwaka jana watu wawe na tabia ya kunawa, wananawa, kutumia vitakasa mikono watu wanafanya na wengine pia wamevaa barakoa, hakuna aliyekataza muhimu aende kwa tahadhari.
“Kwenye mitandao kila mmoja anasema la kwake huko na wale wenye simu ambazo zinaonesha taarifa mbalimbali tumeona Mataifa yakieleza kwamba hii ni vita iliyoanza kwa wakubwa huko na bado wanahangaika nayo sisi Mataifa madogo lazima tuwe makini.
“Tuna Rais wetu makini sana ameendelea kutuongoza vizuri ametusihi tuondoe hofu, lakini muhimu ndani tunaendelea kupambana kuhakikisha kwamba usalama wa watu wetu nchini unaendelea kuwepo barakoa hizo mnazozivaa tulisema ni bora tukajiridhisha,” amesema Majaliwa.