
KUREJEA kwa nyota wake sita ambao walikuwa nje ya kikosi cha Simba wakiongozwa na chaguo namba moja kwa Kocha Mkuu, Didier Gomes, kiungo, Rarry Bwalya, kumeongeza tabasamu kwa kocha huyo.
Bwalya na wachezaji wenzake watano ambao ni Jonas Mkude, Ibrahim Ame, Erasto Nyoni, Kennedy Juma na Ally Salim pamoja na meneja wa timu hiyo, Abas Ally, walibaki DR Congo kwa kile kilichoelezwa na mamlaka kuwa wana maambukizi ya Corona baada ya kumalizana na AS Vita.
Kwa sasa nyota hao tayari wamesharejea Bongo na juzi walianza mazoezi rasmi na wenzao ikiwa ni maandalizi ya mechi yao ya kimataifa ya hatua ya makundi dhidi ya Al Ahly ya Misri.

Kwenye orodha ya wachezaji hao ambao wameungana na timu hiyo, Bwalya amekuwa akipewa nafasi zaidi ambapo mbele ya TP Mazembe alitumia dakika 75, kwa Al Hilal na Dodoma Jiji alimaliza zote 90.
Dhidi ya Azam FC alitumia dakika 78 na AS Vita dakika 59.Jumla kwenye mechi sita ambazo Gomes ameongoza kikosi hicho, amekosekana kwenye mechi moja mbele ya Biashara United na ametumia dakika 392, hivyo kurejea kwake kumeongeza tabasamu kwa Gomes kuelekea mchezo wa keshokutwa Jumanne.
Katika hatua nyingine, Francis Baraza, Kocha Mkuu wa Biashara United, amesema kikosi cha Simba kina uwezo wa kupata matokeo chanya mbele ya Al Ahly ikiwa watacheza kwa nidhamu na utulivu mkubwa.
“Simba wameanza vizuri na wanaweza kupata matokeo chanya kwenye mechi za kimataifa, ila lazima waongeze nidhamu ndani ya uwanja na kupunguza makosa yasiyo ya lazima hasa kwa mabeki pamoja na viungo.
“Ikiwa watakuwa wanaruhusu makosa iwe ndani ya 18 ama karibu na 18 ni hatari kwao kwa kuwa wapinzani wao wanaweza kutumia kila nafasi na kugeuza kuwa bao, hapo umakini unahitaji,” alisema Baraza ambaye aliweka wazi kuwa wachezaji wa Simba wana tabia ya kupoteza muda.
STORI NA LUNYAMADZO MLYUKA | SPOTI XTRA