
RAIS John Magufuli amesema Serikali ina mpango wa kuvunja Jiji la Dar es Salaam na kuchagua manispaa moja katika jiji hilo itakayopandishwa hadi na kuwa Jiji, lengo likiwa kupunguza gharama zisizokuwa za lazima.
ameyasema hayo wakati akizindua Daraja la Juu la Ubungo lililopewa jina la Kijazi, leo Jumatano Februari 24, 2021.
“Ninategemea kuvunja Jiji la Dar es Salaam ili tutengeneze jiji la eneo fulani tunaweza kuifanya Ilala ndiyo iwe jiji, itategemea na namna mambo yatakavyokwenda lakini kuwa na madiwani ambao wanakaa hapa juu wanachangiwa fedha na hawana miradi ya maendeleo hili nitalikataa.
“Tunataka Manispaa moja katika jiji la Dar es Salaam ndiyo ipandishwe hadhi iwe jiji halafu nyingine ziwe manispaa. Jiji la Dar es Salaam litaendelea kuwepo lakini tutachukua eneo fulani na ninafikiri Ilala inafaa kuwa jiji maana ndiyo ipo katikati, Ubungo itasubiri maana barabara bado hazijatengenezwa.
“Wale wanaojiandaa kuwa Mameya wa Jiji la DSM na hawana maeneo wajue hicho kimekwisha, tunataka manispaa moja ya Jiji la DSM ndio ipandishwe hadhi iwe Jiji halafu nyingine ziwe Manispaa, kama kwenye Majiji mengine, mjiandae kisaikolojia waliokuwa wanataka Umeya wa Dar.
“Jiji la Dar es Salaam litaendelea kuwepo lakini tutachukua eneo fulani na nafikiri Ilala inafaa kuwa Jiji kwa sababu ndio katikati ya Mji, Ubungo itasubiri kidogo kwa kuwa hata Barabara bado hazijatengenezwa, lazima tuijenge Dar es Salaam ya kisasa, liwe Jiji kweli la kisasa.
“Haiwezekani unakuwa na madiwani wamekaa tu wanatengewa bajeti hizo fedha ni vizuri zikapelekwa kwenye miradi ya maendeleo ya barabara hayo ni matumizi bora ya fedha za walipakodi kwa hiyo mjiandae kisaikolojia meya atapatikana katika manispaa ya Ilala. Waziri Jafo ameshaniletea drafti nadhani nikimaliza ziara nitaenda kusaini,” amesema Magufuli.