
MBUNGE wa Jimbo la Buchosa, Mhe. Eric Shigongo, amecharuka katika kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Buchosa kutokana na Mamlaka ya Barabara Vijijini (TARURA) kuingia mikataba na baadhi ya wakandarasi wasiokuwa na uwezo na kusababisha ukarabati na ujenzi wa barabara katika Jimbo la Buchosa kushindwa kukamilika kwa wakati na kuharibika mara kwa mara.

Shigongo ametoa wito kwa TARURA kusimamia vyema katika kupata wakandarasi wenye uwezo wa kufanya kazi vizuri kwani hatakubali kuona fedha za Serikali zikiliwa bila kukamilika kwa barabara au barabara zinazojengwa kuwa chini ya kiwango katika Jimbo la Buchosa.

“TARURA licha ya kupewa pesa ndogo na Serikali wamekuwa wakiingia mikataba ya ujenzi wa barabara zetu na watu wasiokuwa na uwezo ama utaalam, mwisho wa siku barabara zetu zinaharibika baada ya muda mfupi tu. Hatuwezi kukubali pesa ya serikali ikapotea, tutagombana na kushindwa kuelewana.

“Huyu mtu hana uwezo, utampaje kazi nyingine. Waheshimiwa madiwani tuwe makini kufuatilia haya. Kama mtu ataona namchongea sawa, lakini mimi ninafanya kazi yangu kwa kuhakikisha miradi ya Serikali inakwenda kama ilivyopangwa. Serikali ifanye ya kwake na TARURA mfanye ya kwenu. Hiyo pesa ya wanyonge mnayopewa muwape kandarasi watu wenye uwezo,” amesema Shigongo.