×

Mastaa 10 wa Simba Kuikosa Kenya

KIM Poulsen, Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars amesema kuwa atakosa huduma za wachezaji 10 wa Simba kwenye mechi za kirafiki dhidi ya Kenya kutokana na wachezaji hao kuwa na kazi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

 

Machi 8, Stars itaingia kambini kwa ajili ya maandalizi ya mechi za kuwania kufuzu Afcon ambapo kabla ya kuvaana na Equatorial Guinea Machi 25 na ule dhidi ya Libya Machi 28, kikosi kinatarajiwa kucheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Kenya.

 

 

Kwenye hizo mechi mbili ambazo zinatarajiwa kucheza Machi 15 na 18, Poulsen atakosa huduma ya nyota wa Simba ambao wamehusika kwenye mabao 25 kati ya 42 yaliyofungwa na timu hiyo ndani ya ligi. Nyota hao ni Shomari Kapombe yeye ni beki wa pembeni ana pasi moja ya bao.

 

 

Erasto Nyoni, Kennedy Juma, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Jonas Mkude, Hassan Dilunga kiungo mshambuliaji ana asisti tatu, ametupia mabao mawili, Mzamiru Yassin kiungo mkabaji ametupia mabao mawili na pasi moja ya bao, Said Ndemla kiungo mkabaji ametupia mabao mawili na ana pasi mbili za mabao, John Bocco yeye ametupia mabao 8 na pasi mbili za mabao na kipa namba moja Aishi Manula.

 

 

Poulsen ameliambia Championi Jumatatu kuwa wachezaji hao wanatarajia kuibuka nchini Kenya mara baada ya kumaliza mchezo wao dhidi ya Al Merrikh, unaotarajiwa kuchezwa Machi 16, Uwanja wa Mkapa.

LUNYAMDZO MLYUKA, Dar es Salaam

Leave a Comment