×

Kilio Katakata ya Umeme Kila Kona

KILIO kila kona. Ndivyo hali ilivyo kutokana na adha ya kukatika umeme kila mahali nchini, hivyo kusababisha wananchi kushindwa kufanya shughuli za maendeleo.

 

 

Hali hiyo imekuwapo kwa takriban wiki moja sasa katika maeneo mbalimbali huku viongozi wa serikali akiwamo Waziri wa Nishati, Dk. Merdard Kalemani, kutaka tatizo hilo limalizike haraka.

 

 

Wakati hali ikiwa hivyo, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limetoa sababu za kukatika kwa umeme na kusema ndani ya siku tano litakuwa limepatiwa ufumbuzi.

 

 

Uchungzi uliofanywa umeonyesha kuwa maeneo mengi ya nchi kuna tatizo hilo ambalo limeathiri kwa kiasi kikubwa utendaji kazi katika sekta za umma na binafsi.

 

 

Mkoani Mbeya, baadhi ya wananchi walisema shughuli zao zimesimama kwa saa kadhaa kutokana na kukosekana kwa umeme wa uhakika, hivyo kupata hasara.

 

 

Maeneo ambayo wananchi wamekuwa wakilalamikia tatizo hilo mara kwa mara ni wilaya ya Mbarali ambayo inatumia njia ya Kongoro, Chunya na baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Kyela.

 

 

Hata hivyo, TANESCO Mkoa wa Mbeya, imekuwa likitoa taarifa mara kwa mara kuhusu kukatika kwa umeme kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo marekebisho ya njia za umeme na hitlafu ya nishati hiyo.

 

 

Taarifa ya TANESCO Mkoa iliyowasilishwa kwenye Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) Januari 6, mwaka huu, ilisema shirika hilo limeomba Sh. bilioni 10.2 kwa ajili ya kuendeleza miradi ya umeme ikiwamo kurekebisha miundombinu.

 

 

PWANI

Mkoani Pwani, wakazi wa maeneo kadhaa hususani Wilaya ya Bagamoyo, wamelalamikia kukatika kwa umeme kila wakati kwa muda mrefu bila taarifa.

 

 

Wamesema hali hiyo imekuwa ikiwaathiri kutokana na kusimama kwa shughuli za kiuchumi, zikiwamo za ujasiriamali na za kijamii, hivyo kuitaka TANESCO kuwa na utaratibu wa kutoa taarifa mapema.

Wiki iliyopita maeneo kadhaa ya Kata ya Mapinga yalikosa umeme kwa zaidi ya siku mbili.

 

 

HOFU MWANZA

Hofu imetanda kwa wafanyabiashara na watumiaji wa umeme katika maeneo mbalimbali jijini Mwanza kutokana na kukatika kwa umeme mara kwa mara bila taarifa yoyote.

 

 

Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi walisema wanalazimika kutumia njia mbadala kunusuru shughuli zao kukwama ikiwamo kutumia jenereta hali inayoongeza gharama katika uendeshaji.

 

 

Mmoja wa wafanyabiashara wa barafu eneo la Kisesa jijini Mwanza, Angel Ben, alisema tatizo la kukatika kwa umeme limeitia dosari biashara yake kwa kuwa barafu zote huyeyuka kila siku umeme unapokatika na kuongeza kuwa hali hiyo imekuwa ikijirudia kwa takriban siku saba sasa.

 

 

Nao baadhi ya wananchi katika maeneo mbalimbali Morogoro, wameomba serikali kutafuta ufumbuzi wa kina na wa haraka juu ya ukatikaji wa umeme tangu mwanzoni mwa mwaka huu bila taarifa na wakati mwingine kwa taarifa.

 

 

Kwa mujibu wa wananchi hao, hali hiyo inaathiri uzalishaji ambao sehemu kubwa unategemea umeme sambamba na kuharibu vifaa vinavyotumia nishati hiyo.

 

 

Baadhi ya wananchi wa maeneo ya Kihonda Mbuyuni, Magorofani, Tushikamane, Mazimbu, Mzumbe, Magadu, SUA na Kasanga, wamelalamikia kukatika huko mara kwa mara kwa umeme bila taarifa na kwamba tatizo hilo limekuwa kero sugu.

 

 

Waliomba utatuzi wa haraka na kwamba badala ya TANESCO kusingizia mvua, radi, miti kuangushwa na upepo, ni vyema ikaweka sawa ratiba kama kuna mgawo wa nishati hiyo.

 

 

“Mbona zamani hali haikuwa hivi? Hata kama ni dharura hizi zimepitiliza maana imekuwa kila siku, usiku na mchana. Umeme unakatika na muda wa kurudi haujulikani. Nimelazimika kuachana na biashara ya samaki kwani ni hasara tupu. Wanaooza unatupa tu hakuna anayekulipa hiyo hasara,” alisema mmoja wa wafanyabiashara wa samaki kutoka Kihonda, Selina Anthony.

 

 

Mwananchi mwingine Twaha Burets akabainisha kinachosikitisha ni wakati mwingine umeme kurudi kwa nguvu kubwa na kuharibu soketi za umeme na vifaa vingine vikiwamo friji na televisheni.

 

 

Naye Adam Mwansele, mkazi wa Kihonda Maghorofani, alisema kwa takribani wiki sasa, huduma za umeme zimekuwa hazipatikani bila shirika hilo kutoa taarifa yoyote kwa wateja. Alisema hatua hiyo imekuwa ikisababisha usumbufu kwa wakazi wa eneo hilo.

 

 

Hassani Kaega, mkazi wa Mazimbu, alisema kukatika kwa umeme katika eneo hilo kumekuwa kukiathiri pia kukosekana kwa maji kwa kuwa maji wanayotumia yanasukumwa na mitambo inayotumia umeme kutoka chanzo cha bwawa la Mindu.

 

 

KILIMANJARO

Wananchi katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Kilimanjaro, wamemtaka Waziri Kalemani kutangaza rasmi mgawo wa umeme lengo likiwa kujipanga namna ya kufanya biashara zao.

 

 

Hamis Ramadhani ni kinyozi katika stendi kuu ya mabasi ya Moshi, alisema ni vyema serikali kupitia TANESCO ikatangaza kama kuna mgawo wa umeme na utachukuwa muda gani kuliko kukata umeme kila siku.

 

 

“Kwa sasa TANESCO mkoani hapa wanakata umeme hata mara tano kwa siku bila taarifa yoyote na zaidi kabisa hakuna taarifa za ukataji wa umeme huo. Unaweza kukatika hata zaidi ya saa nane,” alisema.

 

 

Naye Samwel Msuya, mfanyabiashara wa samaki katika soko kuu la kati, Manispaa ya Moshi, alisema kwa takribani mwezi mmoja umeme umekuwa ukikatika kila mara.

 

 

“Viongozi wa TANESCO Kilimanjaro si wasikivu na huwatolewa wateja lugha zisizo na staa. Unatoa taarifa ya kukatika kwa umeme hakuna ufuatiliaji. Nimeunguliwa na mafriji mawili na sasa nashindwa kuagiza mzigo wowote kutokana na hali hiyo,” alisema Msuya.

 

 

DODOMA SAFI

Wakati hali ikiwa ya wasiwasi katika mikoa mbalimbali, mkoani Dodoma hakuna mgawo wala tatizo la umeme isipokuwa kumekuwapo na tatizo la kukatika kwa baadhi ya laini kutokana na matengenezo madogo na baadaye umeme hurejeshwa.

 

 

Ofisa Habari wa TANESCO Mkoa wa Dodoma, Innocent Lupenza, alisema kwa mkoa huo hakuna tatizo la umeme na kama kuna katizo lolote taarifa hutolewa.

 

 

“Hakuna tatizo la umeme kama labda kuna laini umekatika tangazo linatolewa na ni matengenezo ya muda na baadaye kurejeshwa,” alisema.

 

 

Imeandikwa na Grace Mwakalinga (MBEYA), Mary Mosha (MOSHI), Idda Mushi na Ashton Balaigwa (MOROGORO) na Elizabeth Faustine (Mwanza).

Leave a Comment