


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo Machi 4, 2021 amefungua na kufunga mkutano Mkuu wa tatu wa Wanawake katika Uongozi kwa mwaka 2021 na Mahafali ya 4,5,6 ya Programu ya Mwanamke wa Wakati Ujao katika Ukumbi wa Serena Jijini Dar es salaam, ambapo kauli mbiu ya mkutano huo ni “Ukuzaji wa Vipaji vya Mwanamke walio katika Uongozi ili kuwa na Mashirika Endelevu”.
HOTUBA YA MHESHIMIWA SAMIA SULUHU HASSAN, MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KATIKA MKUTANO MKUU WA TATU WA WANAWAKE KATIKA UONGOZI KWA MWAKA 2021 NA MAHAFALI YA 4, 5 & 6 YA PROGRAMU YA MWANAMKE WA WAKATI UJAO, TAREHE 04 MACHI, 2021
HOTELI YA SERENA, JIJINI DAR ES SALAAM
Mheshimiwa Jenista Mhagama (Mb.), Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu;
Bi Jayne Nyimbo Taylor, Mwenyekiti wa ATE;
Mheshimiwa Elisabeth Jacobsen, Balozi wa Norway nchini Tanzania;
Bwana Wellington Chibebe, Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani Ofisi ya Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi;
Bwana Felix Kagisa, Makamu Mwenyekiti wa ATE;
Waheshimiwa Wajumbe wa Bodi ya ATE;
Dr. Aggrey K. Mlimuka, Mkurugenzi Mtendaji wa ATE;
Wakurugenzi wa Makampuni;
Maafisa Watendaji Wakuu;
Wataalamu Waelekezi kutoka Chuo cha ESAMI;
Washiriki wa Awamu ya Nne, Tano na Sita ya Mafunzo ya Programu ya Mwanamke Kiongozi;
Ndugu Wageni Waalikwa;
Waandishi wa Habari,
Mabibi na Mabwana,
Habari za Asubuhi.
Niungane na walionitangulia kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza kujumuika nanyi katika Mkutano Mkuu wa Tatu wa Wanawake katika Uongozi ulioambatana na Mahafali ya Nne, Tano na Sita ya Programu ya Mwanamke wa Wakati Ujao.
Nawashukuru sana waandaji ATE kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Waajiri Nchini Norway (NHO) pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu. Hii ni mara yangu ya pili kuhudhuria uzinduzi wa Programu, mwaka 2016 pia nilifanya shughuli hii. Asanteni kwa imani kubwa mliyonayo kwangu na kwa Serikali ya Awamu ya Tano.
Nina taarifa kuwa kwa miaka mitatu mfululizo mmefanikiwa kuandaa Mkutano huu Mkuu wa Mwaka wa Uongozi kwa Wanawake ambao unaenda sambamba kabisa na juhudi za Serikali za kuhakikisha idadi ya wanawake katika nafasi za juu za uongozi inazidi kuongezeka, na pia kuwa na idadi kubwa ya wanawake katika Bodi za Wakurugenzi za makampuni mbalimbali.
Mchango wa ATE katika kukuza na kuboresha uchumi wa Taifa letu ni mkubwa. Serikali inathamini na kutambua mchango huu na tumejipanga vizuri kuhakikisha tunafanya kazi pamoja. Kauli mbiu yetu ya “HAPA KAZI TU” inatuagiza kufanya kazi kwa kushirikiana na wadau wote ili kuweza kufikia lengo la Agenda ya Afrika 2063 ya Afrika tuitakayo yenye Maendeleo Endelevu na Ukuaji wa Uchumi Unayomshirikisha kila Mtu (The Africa we want: Inclusive & Sustainable Economic Growth and Development).
Hata hivyo, katika hatua za haraka Serikali inajitahidi kuendana na wito wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia (SDGs) ya kwenda na safari ya maendeleo bila kumuacha mtu nyuma ifikapo mwaka 2025. Katika safari ndefu ya maendeleo, tulifanikiwa kufikia uchumi wa kati katika awamu hii, si kutokana na juhudi za Serikali pekee, ila ni pamoja na michango ya wadau wengi, mkiwemo ATE mkishirikiana na waajiri na waajiriwa katika kuchapa kazi kwa ufanisi na tija kwa ajili ya maendeleo ya nchi na jamii yetu.
Mwenyekiti ATE, Mabibi na Mabwana,
Kwa jambo hili lililotukusanya leo, nakupongezeni sana ATE kwa kushirikiana na Chuo cha ESAMI kwa kuhitimisha mafunzo ya Awamu ya Nne, Tano na Sita ya Mwanamke wa Wakati Ujao kwa mafanikio makubwa. Kama nilivyosema hapo awali nilishiriki uzinduzi wa programu hii mnamo mwaka 2016 na nimefurahi sana kuona kwamba mafunzo haya yamekuwa endelevu na idadi ya wanawake imeongezeka hadi kufikia wanawake 150 na kupelekea kutengenezwa kwa alumni ya wanawake waliopitia mafunzo haya.
Hii imenipa faraja kubwa na imani juu ya nia thabiti ya ATE katika kushirikiana na Serikali kuhakikisha tunafikia usawa wa kijinsia (asilimia 50 kwa 50) katika nafasi za juu za uongozi wa makampuni na katika bodi mbalimbali.
Nazipongeza kampuni zote ambazo zimefanikisha kuleta wafanyakazi wao katika Awamu ya Nne, Tano na Sita ya mafunzo ya programu hii yenye lengo la kuwajengea uwezo wanawake ili waweze kushika nafasi za juu za uongozi na kuwapa uwezo wa kuingia kwenye bodi mbalimbali na kushiriki katika kutoa maamuzi. Ni jambo la kutia moyo kwamba wanawake kadhaa waliohitimu programu hii tayari wamefanikiwa kupata nafasi za juu za uongozi na pia kuwa wajumbe kwenye bodi mbalimbali huku mchango wao ukionekana dhahiri.
Mwenyekiti ATE, Mabibi na Mabwana,
Nimefurahishwa sana na kaulimbiu ya Mkutano huu inayosema “Ukuzaji wa Vipawa vya Wanawake Walio Katika Uongozi ili Kuwa na Mashirika Endelevu.” Mada hii imekuja wakati muafaka kwani kama taifa tunapaswa kujadili kwa kina kuona ni jinsi gani tunahakikisha wanawake zaidi wanajikita katika uongozi, na kuhakikisha vipaji vyao vya uongozi vinahamasishwa na kutumika kwa maendeleo endelevu, sio tuu ya Taasisi wanazoongoza bali ya jamii nzima. Kwa kipindi cha hivi karibuni wanawake wengi wameonesha umahiri mkubwa katika uongozi, hususan katika nafasi za juu wanazoaminiwa. Ukuzaji wa vipawa na mafunzo kama haya ya “Mwanamke Kiongozi” yamekuwa chachu katika kulea, kuandaa na kukuza wanawake wenye upeo wa kitaaluma na uwezo mkubwa wa kazi ambao wameleta ufanisi mkubwa kwenye uongozi na Tija katika Makampuni yao.
Mwenyekiti ATE, Mabibi na Mabwana,
Tafiti mbalimbali zinaonesha kwamba ushirikishwaji wa wanawake katika nafasi za juu za uongozi wa makampuni huongeza ufanisi sehemu za kazi na kupelekea kuongezeka kwa uzalishaji. Aidha, Ripoti ya Mwaka 2019 ya Shirika la Kazi Dunia (ILO) iliyokuwa na kichwa cha Habari ‘Wanawake Katika Biashara na Usimamizi’ ilibainisha kuwa kampuni za kibiashara zenye uwiano mzuri wa jinsia kwa kuwapa fursa sawa wanawake na wanaume katika ngazi ya juu ya uongozi zinafanya vizuri katika shughuli zao ikiwemo kupata faida kubwa. Takribani robo tatu ya kampuni hizo ziliripoti ongezeko la faida kati ya asilimia 5 hadi 20. Makampuni hayo pia yalifanikiwa kuongeza ubunifu na uwazi huku wakifanikiwa kuwa na uwezo wa kuvutia na kuendeleza wafanyakazi wenye vipaji, ubunifu na uwazi (transparent) katika kutekeleza majukumu yao. Hata hivyo, ripoti hiyo inasema faida ya uwiano mzuri wa kijinsia inaanza kuonekana pale ambapo wanawake wanashikilia asilimia 30 ya ngazi za juu za uongozi.
Kwa bahati mbaya takribani asilimia 60 ya makampuni hayafikii lengo hilo la kuwa na uwiano mzuri wa kijinsia katika ngazi za juu za uongozi. Haya ni matokeo ya mambo mbalimbali kama changamoto za elimu, kukosekana kwa sera madhubuti sehemu za kazi na utamaduni wa mfumo dume katika makampuni ambao unakwamisha wanawake kupata nafasi nyingi zaidi. Ni wazi kuwa bado tuna kibarua kigumu ili kufikia malengo haya. Nipende kuhimiza taasisi, makampuni na wadau mbalimbali mliopo hapa kufanya jitihada mbalimbali na kushirikiana pamoja kuongeza idadi ya wanawake katika nafasi za juu za uongozi ili kupata mafanikio yaliyotajwa katika ripoti hiyo.
Naamini mkutano wa mwaka huu utatumika kama fursa ya kuyaonesha Makampuni na Taasisi mbalimbali njia bora za kukuza vipawa vya wanawake walio katika nafasi za chini na za kati za uongozi ili waweze kupanda na kushika nafasi za juu. Ni matumaini yangu tutapata pia uzoefu kutoka taasisi mbalimbali na kuja na mpango kazi utakaoainisha, mapungufu, changamoto, nafasi za Serikali, Wanawake, ATE na wadau wote husika katika kukuza na kuhakikisha wanawake wenye uzoefu, (uzalendo – hakuna shaka) na wachapakazi wanaweza kupatikana kuchukua nafasi za uongozi. (Je kila mwanamme aliyeshika nafasi za juu ana sifa hizo?) Kwanini Mwanamke apate mafunzo ya ziada wakati walihitimu vizuri sawa na Mwanamme (Tuangalie root cause) na kwa nini kusiwe na Mafunzo kwa Wanaume kuwatoa hiyo kasumba kwamba mwanamke ni mdhaifu mpaka apate mafunzo ya ziada? Tunafundisha nini hasa peculiar kwa mwanamke ambacho Mwanamme hahitaji? Haya na Kutokujiamini!!!!!!!!
Ni matumaini yangu kuwa mpango kazi huu utajumuisha si tu wale watumishi walio kwenye ajira rasmi bali pia tuangalie ni namna gani tunaweza kuwalea wanawake katika sekta isiyo rasmi. Kuna msemo wa Udongo upate ulimaji, msemo huu unatupeleka kuona ni kwa namna gani watoto kuanzia shule za msingi au sekondari tunawakuza waweze kushika nafasi za uongozi. Ili kuhakikisha suala hili linakuwa endelevu ni lazima kuwe na mpango kwa ninyi Wanawake mnaohitimu, kulea klabu za aina hio mashuleni. (Mentorship programmes).
Tuacheni hulka mbaya ya adui wa mwanamke ni mwanamke mwenzie au ule mtindo wa kuwa mwanamke akiwa juu kutumia mfumo wa PHD (Pull Her Down). Wakati umefika sasa tukaungana kwa pamoja kuvunja glass ceiling na kusema tunaweza, tutashikana na kusaidiana.
Mwenyekiti ATE, Mabibi na Mabwana,
Serikali yenu inajidhatiti kuutekeleza Mpango Mkakati wa Kitaifa kwa ajili ya Maendeleo ya Usawa wa Kijinsia ambao upo kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025, pamoja na mipango ya Afrika na Dunia niliyoitaja hapo awali, kuhakikisha kunakuwa na uwiano wa kijinsia katika shughuli za kiuchumi, elimu, mafunzo mbalimbali na ajira katika nyanja zote.
Sisi tuliobahatika kushika nafasi za juu katika maeneo mbali mbali tunapaswa kushirikiana kwa pamoja katika kutambua na kuibua karama/talanta mbalimbali za Uongozi zilizopo ndani ya wanawake na kuwajengea ujasiri ili tuzidi kuona wengi zaidi wakithubutu na kushiriki katika uongozi. Mtakubaliana na mimi kwamba pamoja na kuongezeka kwa Idadi ya Wanawake waliopo kwenye nafasi za juu za Uongozi bado tunahitajika kufanya kazi kwa bidii na kuweka mipango madhubuti kuhakikisha malengo ya uwiano wa kijinsia tuliyojiwekea yanafanikiwa. Nipende kutoa rai yangu kwa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Taasisi mbalimbali za kibiashara na Wadau mbalimbali nchini kuungana na sisi ili kuhakikisha programu hii inakuwa endelevu kwa kuwahamasisha wanawake wengi kushiriki mafunzo haya.
Mwenyekiti ATE, Mabibi na Mabwana,
Nawapongeza Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kwa mafanikio haya makubwa ya kutoa mfunzo kwa Wanawake kutoka kampuni mbalimbali katika Awamu hizi tatu ya Programu hii ya Mwanamke Kiongozi kwani imekuwa ni sehemu ya kuongeza Wanawake wengi zaidi katika nafasi za uongozi na uwakilishi katika Bodi za Wakurugenzi katika Taasisi mbalimbali. Pia nizipongeze kampuni mbalimbali zilizowekeza katika kuhakikisha wanakuza vipawa vya wafanyakazi wanawake katika kampuni zao. Zaidi kabisa niwapongeze kina mama ambao wamefanya jitihada binafsi kushiriki mafunzo haya. Nitoe Indhari kwamba (1. Mafunzo isiwe ndio sharti pekee na 2. Mafunzo hujenga tamaa, anapohitimu wasiwekwe sana).
Mwenyekiti ATE, Mabibi na Mabwana,
Nipende pia kuwahamasisha wanawake wengi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Programu hii kwani imekuwa na mchango chanya katika maeneo mbalimbali ya kazi, katika jamii wakiwa kama viongozi, wananchi na pia kama Mama, Wake, Dada na washiriki wakubwa wa kujenga taifa letu. Nataka nisisitize kwamba pamoja na yote ya kumjenga mwanamke aweze kufikia tunapopataka, Waajiri vile vile, lazima waitambue na kuiheshimu nafasi ya mwanamke pahala pa kazi na katika jamii ya Kitanzania.
Pia nitoe rai kwa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kushirikiana na taasisi nyengine zaidi ya taasisi wanachama wao, kueneza mafunzo haya ili kukuza vipaji katika taasisi hizo kwa manufaa ya nchi kwa ujumla. Ningependa kuona mafunzo haya yanawafikia hata viongozi wanawake walio katika Serikali yetu, Wabunge wanawake, Madiwani na hata Maafisa wengine wakuu wa Serikali ili kuhakikisha wote tunajenga mwelekeo mmoja.
Mwenyekiti ATE, Mabibi na Mabwana,
Nihitimishe hotuba yangu kwa kuwapongeza tena ATE ambao wameshirikiana na Shirikisho la Vyama vya Waajiri Nchini Norway (NHO) kwa kuandaa mkutano huu kwa ustadi wa hali ya juu na ninaamini utaleta mafanikio makubwa kwa manufaa ya wanawake wengi wenye ndoto za kuwa viongozi na kupelekea matokeo chanya kwa taifa letu kwa ujumla.
Nichukue sasa nafasi hii kutamka rasmi kuwa Mkutano Mkuu wa Tatu wa Wanawake katika Uongozi kwa Mwaka 2021 umefunguliwa Rasmi pia na Wahitimu wote wa Awamu ya nne, tano na sita ya Mafunzo ya Mwanamke Kiongozi inayoratibiwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) wamehitimu rasmi.