
CHAMA cha ACT Wazalendo kimesema kutokana na uzoefu waliokuwa nao kwenye chaguzi za Serikali za Mitaa, walikuwa hawaamini kama wagombea wao wangepitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, ndiyo maana walipeleka majina ya Bernard Membe (ACT) na Tundu Lissu (Chadema), wakati mazungumzo yakiendelea ili yeyote atakayepitishwa wamuunge mkono.
Hayo yamesemwa leo na katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu wakati akifanya mahojiano maalum na Kipindi cha Front Page kupitia Global Radio leo Ijumaa, Machi 5, 2021.
“Tulipoafikiana kumuunga mkono Lissu kwenye urais, Membe alikuwa na mawazo tofauti, akasema siwezi kuvunja Sheria ya nchi, akasema hata nikijitoa au nisijitoe haina tifauti sababu muda wa kujitoa umeshapita na kura zitapigwa na kuhesabiwa, ndio mpishano uliokuwepo.

“Funzo tunalolipata kuhusu Bernard Membe huko mbeleni ni kufanya maamuzi mapema. Hata kwenye UKAWA 2015 mambo kama haya yalikuwepo. Haya makubaliano ya nani agombee wapi, yanapaswa kumalizika mapema.
“Siwezi kuzungumzia suala la Lowassa 2015 sababu sisi hatukuwa sehemu ya UKAWA. 2020 ACT tulimchambua Membe tukaona yeye ni kama lebo, tukamuona ni mwanasiasa mzuri na baada ya uchaguzi 2015 wenzake walikubaliana na chama chao lakini membe amekuwa akikinzana nao.
“Ifike wakati vyama vya upinzani tutafakari kwa kina kuwa hakuna haja ya kuwapa watu wanaotoka CCM kuhamia kwetu hivi karibuni nafasi za kugombea urais. Upinzani tujiandae mapema ili tusisombwe na matukio na mwenendo wa mambo ndani ya CCM, Membe na Lowassa watufunze,” amesema Ado Shaibu.