×

SBL yatoa ufadhili wa masomo ya kilimo kwa wanafunzi wengine 70

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bia ya Serengeti Mark Ocitti (kulia) akiongea na wanafunzi wa chuo cha Kaole Wazazi College of Agriculture cha Bagamoyo mkoani pwani ambao ni wanufaika wa program ya ufadhili wa masomo walipotembelea kiwanda cha kampuni hiyo cha Dar es Salaam. Kushoto ni Makamu mkuu wa chuo hicho Maximillian Sarakiky

Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) leo imetangaza kutoa nafasi mpya 70 za ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wanaosomea kilimo hapa nchini. Ufadhili huu unajumuisha ada pamoja na gharama nyingine zote za masomo katika kipindi chote mwanafunzi anapokuwa chuoni.

Hii ni mara ya pili kampuni ya SBL inatoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo yao na ambao wanatoka katika familia zenye vipato duni. Mwaka jana wakati SBL ikizindua mpango wake wa ufadhili wa masomo ya kilimo unaojulikana kama Kilimo Viwanda, ilitoa ufadhili kwa wanafunzi 40.

Programu ya Kilimo-Viwanda inalenga kuunga mkono jitihada za serikali katika kuongeza idadi ya wataalamu wa kilimo hapa nchini, kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa SBL, Mark Ocitti

Akitangaza wanafunzi 15 waliopata ufadhili huo kwa mwaka huu kutoka chuo cha Kaole Wazazi College of Agriculture cha Bagamoyo mkoani Pwani, Ocitti alisema pamoja na kutoa ufadhili wa masomo kampuni hiyo pia inafanya kazi na wakulima 400 ambao mwaka jana waliiuzia SBL tani 17,000 za nafaka sawa na asilimia 70 ya mahitaji yake ya malighafi kwa ajili ya kutengenezea bia.

Baadhi ya wanafunzi wa chuo cha Kaole Wazazi College of Agriculture cha Bagamoyo mkoani pwani wakifuatilia mada zilizokuwa zinatolewa walipotembelea kiwanda cha kampuni hiyo

“Uhusiano wa SBL na sekta ya kilimo una historia ndefu. Kwa sasa kampuni inafanya kazi na mtandao wa wakulima 400 kwenye mikoa nane hapa nchini ambapo tunanunua shayiri, mahindi na mtama kwa ajili ya uzalishaji wa bia zetu. SBL huwasaidia wakulima hawa kwa kuwapatia mbegu za bure, huduma za ughani pamoja na kuwaunganisha na taasisi za kifedha kwa ajili ya kupata mikopo na kupanua uzalishaji wao,” alisema.

Mkuu wa chuo cha Kaole Wazazi College of Agriculture, Sinani Simba, aliishukuru kampuni ya SBL kwa kuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono maendelea ya sekta ya kilimo ambayo ni sekta mama inayoajiri Watanzania wengi kuliko sekta nyingine yeyote ile.

Meneja Afya na Usalama wa Kampuni ya Bia ya Serengeti David Mwakalobo (kulia) akifafanua jambo kwa wanafunzi wa chuo cha Kaole Wazazi College of Agriculture cha Bagamoyo mkoani pwani

“Mafunzo kwa ajili ya wataalamu wa kilimo ni moja kati ya vipaumbele kwenye Mpango wa Maendeleo ya Kilimo Awamu ya Pili. Wataalamu wa kilimo ni muhimu katika kuwasaidia wakulima kuboresha shughuli zao kwa kuwaelekeza namna ya kulima kitaalamu ili kuongeza uzalishaji na kuboresha vipato vyao,” alisema mkuu huyo wa chuo.

Mmoja wa wanafunzi ambaye ni mnufaika wa programu ya ufadhili wa masomo,Emmanueli Ntandu,Akifafanua jambo

Kampuni ya SBL inashirikiana na vyuo vinne vya hapa nchini katika kutoa iufadhili wa masomo chini ya Programu ya Kilimo Viwanda. Pamoja na Kaole Wazazi College of Agricultre, vyuo vingine ni pamoja na chuo cha Kilacha Agriculture Institute kilichopo Moshi mkoani Kilimanjaro, Igabiro Institute of Agriculture kilichopo Bukoba mkoani Kagera na St. Maria Goretti Agriculture Training Institute kilichopo mkoani Iringa.

 

 

 

 

Leave a Comment