
Jeshi la Polisi linamshikilia mkazi wa kwa Mustafa jijini Dar es Salaam, Lucas Joseph kwa tuhuma za kukutwa na kete 226 za dawa za kulevya aina ya bangi. Mtuhumiwa huyo anadaiwa kuwa alikuwa amezificha dawa hizo kwenye shimo la taka nyumbani kwake.
Akizungumza na Mawananchi Machi 6, 2021 Kamanda wa Polisi jijini Ilala, Janeth Magomi amesema Joseph anadaiwa ni mfanyabiashara mkubwa wa dawa za kulevya na alikamatwa akiwa na kete hizo 226.
Kamanda Magomi amesema mtuhumiwa huyo alipohojiwa alikiri kujihusisha na biashara hiyo kwa muda mrefu sasa. “Ni kweli mtuhumiwa huyo tunamshikilia na yupo Kituo cha Polisi Stakishari- Ukonga, tunaendelea kumuhoji ili kubaini mtandao mzima na tukikamilisha upelelezi basi atafikishwa mahakamani,” amesema Kamanda Magomi.
Kwa upande wake kiongozi wa shirika la ulinzi eneo la Chanika, Shaban Mtatula amesema awali walibaini mionendo isiyokuwa ya kawaida nyumbani kwa mtuhumiwa huyo.