
ASANTE Allah kwa Ijumaa nyingine kareem! Rafiki yangu, leo ngoja nikuambie kitu muhimu; kwamba mazoea huleta kukinai na hili lipo sana kwenye uhusiano wa kimapenzi. Kwamba; kila afanyalo mpenzi wako, wewe unahisi kichefuchefu tu.
Unatamani aondoke kwenye maisha yako, angalau upate kupumua. Inapofikia hatua hii, unaweza ukahisi umemchoka mpenzi wako.Unaweza kujikuta umeanza kufikiria mwenzako uliyenaye, siyo sahihi kwako na hutaki kuendelea naye.
Ukijisikia hivi, usishangae au kujilaumu sana, kwani ni kawaida kwenye uhusiano kujisikia hivi wakati mwingine. Nitakayozungumza hapa leo hayawahusu sana wanandoa, bali akina dada walio kwenye uhusiano wa kawaida wa kimapenzi.Mapenzi ni hisia za ndani.
Uamuzi wa kuendelea na mtu katika hatua ya uchumba ambayo huambatana na ndoa ni wa mhusika mwenyewe. Hakuna atakayekushikia fimbo au kukulazimisha umpende au usimpende mtu fulani.Mnapokuwa kwenye uhusiano ni kipindi chenu cha kuchunguzana vizuri.
Kila mmoja lazima amjue mwenzake sawasawa. Hii itamsaidia kila mmoja kufahamu anakwenda kuingia kwenye ndoa na mtu wa aina gani. Lakini aghalabu hutokea unahisi huwezi kuendelea tena na uhusiano na mwenzako na kwamba wakati umewadia wa kuachana.
Huwenda umegundua kwamba mwenzako hakufai kwa sababu zako binafsi ambazo kwa hakika huwezi kumweleza. Lakini ukitafakari jinsi ya kuachana naye, mwenzako anakuwa amekolea kwa upendo kwako. Inawezekana umejaribu kupima sababu zako na ukagundua hazina uzito au siyo za msingi.
Sababu ambazo huwezi kumwambia mpenzi wako, lakini moyo umekuthibitishia kwamba huyo si chaguo lako na uking’ang’ania kuendelea naye, basi furaha kwenye maisha yako itakuwa ni sawa na kitendawili kigumu mno.Hali hii ni ya kawaida na mara nyingi suluhisho lake siyo kuachana na mwenzako kwa jazba, bali inabidi ufanye tathmini.
Ni muhimu ujiulize kwa nini unataka kumwacha mwenzako. Hii ni hatua ya kwanza na muhimu. Kama nilivyosema awali, ni vyema kuuchunguza moyo wako, maana usije ukamwacha kwa sababu ya tamaa zako au umeleweshwa penzi na mwingine, ukashawishika.
Ikiwa hizi ndizo sababu zako, unajiweka katika hali ya utata na baadaye unaweza kujutia hatua yako. Sababu kubwa ya kuachana kwenu inatakiwa iwe ile ya kutafuta amani ya moyo wako, maana umejichunguza na umegundua kwamba, kulazimisha kuendelea naye, maana yake utaishi maisha yasiyo na amani.
Kama ndivyo, wazo hili ni sahihi, lakini kumbuka hutakiwi kumuumiza mwenzako wakati ukitekeleza jambo hili ambalo ni matakwa yako binafsi. Jiulize kama hizi sababu zinazungumzika.
Zipo sababu kuu mbili za kutaka kusitisha uhusiano; ya kwanza nilishaifafanua kwenye kipengele kilichotangulia, lakini ya pili sasa ni kama kweli ana kasoro ambazo unaweza kumweleza moja kwa moja.
Kumbuka njia nitakazokueleza hapa ni za muda mrefu, zinahitaji ufundi na inategemea na namna mwenzako atakavyopokea, hivyo kama unajua mwenzako hajatulia na ushahidi unao, zungumza naye waziwazi kuliko kumzungusha.
Ukishayatenda hayo yaliyotangulia, punguza naye mawasiliano. Kumbuka, silaha ya kwanza ya penzi lako ni mawasiliano. Kuwasiliana ndiko kunapodumisha penzi au kuliporomosha. Punguza kumpigia simu au kumwandikia ujumbe mfupi.
Akikupigia yeye pokea, akituma ujumbe mfupi, unaweza kujibu na wakati mwingine kuacha kujibu. Akikuuliza, mwambie una mambo mengi. Hii ni alama ya kwanza itakayomfanya ahisi uhusiano wenu umeanza kuyumba.
Ni muhimu utambue kwamba kuachana na mtu uliyempenda kwa dhati ni mtihani mgumu, unahitaji kuamua na kujitolea kwani bila hivyo utajikuta ukiyumba huku na kule. Hata hivyo, pia ujue hisia ya kumchoka mwenzako ni ya kawaida na wakati mwingine suluhisho siyo kuachana naye, bali kutathmini tofauti zilizojitokeza na kuzipatia suluhu.
Rafiki kwa leo ninaishia hapa, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine murua kabisa!