
AHADI mojawapo ya kiserikali ambayo inatekelezwa hadi sasa, ni kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara na wajasiriamali, yatakayowasaidia kuendesha viwanda, ikiaminika ndio mwarobaini wa kuliinua taifa kiuchumi.
Ni hali inayofungua milango ya ajira na misukumo mingine ya maendeleo, kulingana na mitaji, ujuzi na ngazi za tofauti kielimu.
Tayari kuna asasi mpya na za kale, kutoka ndani na nje ya nchi zinahamasika kushiriki maendeleo ya taifa, ikiwamo Shirika lisilo la Serikali Mikono Yetu, jijini Mwanza, lililojikita kuwawezesha kinamama kumiliki rasilimali zalishi, kama ardhi na mifugo wajikwamue.
Mikono Yetu inajenga kiwanda mahsusi cha wanawake katika Kata ya Kahumulo, wilayani Sengerema, mkoani Mwanza, pamoja na kuwatengea eneo la soko.
Meneja Programu wa Mikono Yetu, Sophia Nshushi, anasema ni kiwanda kitakachochakata bidhaa za mifugo na mazao kilimo, kwa matarajio ya kunufaisha wanawake zaidi ya 150, ikigharimu Sh. milioni 30.
Anasema, waliamua kujenga katika kata ya Kahumulo, kwa sababu asilimia kubwa ya kinamama wanaishi vijijini na anaendelea:
“Hadi sasa tuna jumla ya shilingi milioni 15, ambazo tumezipata kutoka Shirika la Kimataifa la Women First International Fund, lililoko nchini Marekani na shirika lisilo la kierikali linalotetea haki za wanawake (Kivulini) lenye makao yake jijini Mwanza.”
INAVYOJENGWA
Katika ujenzi, anafafaua kinamama ndio wanashiriki majukumu ya usaidizi kama kuchota maji, kuchanganya mchanga na saruji na kuwasadia mafundi, lengo ni kuwajengea hisia za umiliki halali, pale kitakapoanza uzalishaji.
“Waweze kuwa wabunifu zaidi katika bidhaa watakazozalisha. Lengo la Shirika la Mikono Yetu ni kukuza biashara za kinamama kwa kuzirasimisha,” anaendelea Sophia.
MCHANGO WA SIDO
Sophia anasema waliwapeleka wanawake 14 katika Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) mkoa wa Mwanza, wakafunzwe stadi za ujasiriamali, na usindikaji aina ya vyakula na matunda 130.
Anaeleza, Mikono Yetu inaamini mwanamke atakapomilikishwa rasilimali zalishi, anaondokana na ukatili katika jamii yake.
Meneja wa SIDO mkoani Mwanza, Bakari Songwe, anasema kiwanda tarajiwa kinakidhi viwango vya kiserikali, hivyo wataendelea kuwapa mafunzo na kuwaunganisha na taasisi mbalimbali za wanawake, wafanye na biashara yenye tija.
Katibu wa wanawake hao, Ankres Paulo, anasema wanatarajia kiwanda kitawaongezea kipato kupitia mazao ya mifugo, ikiwamo ng’ombe.
“Sengerema ina viwanda vingi ambavyo vinachakata mazao mbalimbali ya chakula, lakini hakuna kiwanda kinachochakata mazao ya mifugo, yakiwamo maziwa.
“Hali hiyo ilitukosesha fursa za kujiongezea kipato, maana wanawake wengi wa eneo hili tunajishughulisha na ufugaji,” anasema.
Katibu huyo anasema katoka kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani wiki hii, waliendesha ‘harambee’ iliyowashirikisha wanufaika wote, wakapata Sh. 300,000, zitakazowasaidia kwenye ujenzi wa kiwanda.
“Kwetu sisi kiasi hicho ni kikubwa tutakuwa tunafanya hivyo mara kwa mara. Bado inahitajika shilingi milioni 10, ili ujenzi ukamilike.
“Tunawaomba wadau mbalimbali watakaoguswa watusaidie, Shirika la Mikono Yetu limetusaidia sana, sisi tunaendelea pia kujitoa katika shughuli mbalimbali za ujenzi kwa zaidi ya asilimia 70.
WANUFAIKA
Wanufaika Secilia Medadi, Yunia Misana na Rachel Thomas, wana mtazamo kwanza kitakapokamilika kitasaidia kuwainua kiuchumi familia zao.
“Naamini uwapo wa bidhaa za aina mbalimbali sokoni ambazo tutazizalisha kiwandani, utasaidia kupata wageni wengi kutoka maeneo mbalimbali, ambao watasaidia kata yetu kuwa kitovu cha biashara ndani ya wilaya hii,” anasema Secilia.
Rachel, ana mtazamo kiwanda kitamsaidia kusindika mazao yake ya chakula kutoka shambani yaliyokuwa yanaharibika.
“Huwa najishughulisha na kilimo cha nyanya. Kama unavyojua zao hilo, linawahi kuharibika. Kabla sijapata mafunzo ya usindikaji kutoka SIDO, nilikuwa nikikosa wateja, nyanya nyingi zilikuwa zinaharibika au inabidi nizigawe kwa majirani.
“Tangu nimepata mafunzo nimeanza kusindika, shauku yangu ni kuona kiwanda kinaanza ili nifanye kazi hiyo kwa tija zaidi,” anasema.
Yunia Misana, anasema kiwanda tarajiwa kitawakomboa wanawake wanaojishughulisha na kilimo katika kata hiyo, kwa sababu awali walikosa utaalamu wa kusindika.
SERIKALI MTAA
Diwani wa Kata ya Kahumulo, Fortunatus Nzwagi, anaunangalia mradi huo katika sura ya chachu ya maendeleo kwa wakazi wake, kwani jamii sasa itawezeshwa kupitia mwanamke anayeinuka.
Ofisa Mtendaji wa Kata hiyo, Kepha Chima, anaomba wadau na asasi zingine kwenda kuwekeza katika eneo hilo, kutokana na uhalisia wa rutuba yake.