
RAIS wa Rwanda, Paul Kagame na mkewe Jeannette Kagame wamepokea chanjo ya corona katika Hospitali ya Mfalme Faisal jana Alhamisi, Machi 11, 2021.
Kagame amesema zaidi ya watu 230,000 wamepatiwa chanjo katika zoezi hilo linaloendelea nchini humo. Kagame amekuwa Rais wa kwanza katika Ukanda wa Afrika Mashariki kupata chanjo ya Covid19 wakati zoezi hilo likiendelea kwa kasi katika baadhi ya mataifa ya Afrika.
Picha za Kagame (63) na mkewe, wakipatiwa chanjo katika mjini Kigali zimepostiwa kwenye akaunti yake ya Twitter na kusambaa kwenye mitandao mbalimbali na vyombo vya habari nchini humo.
Jina la chanjo ambayo Kagame na mkewe wamechanjwa haijatajwa hadharani lakini tayari nchi hiyo imeshapokea dozi 100,000 ya chanjo za Pfizer-BioNTech na dozi 240,000 za AstraZeneca.

Rwanda, ni nchi yenye watu milioni 12 ambapo imepanga kutoa kinga kwa asilimia 60 ya watu wake ndani ya mwaka huu na kufikia asilimia 60 ya watu wote ifikapo mwisho wa mwaka 2022.
Mwishoni mwa mwezi Februari, Rwanda ilikuwa nchi ya kwanza katika Ukanda wa Afrika Mashariki kuanza kutoa chanjo ya Covid19 kwa wananchi wake kwa kutumia kinga ya Moderna kuwachanja watu ambao walikuwa katika hatari kubwa ya kuambukizwa wakiwemo wafanyakazi wa sekta ya afya.
Rwanda imeshafanya vipimo zaidi ya milioni moja na kubaini takribani kesi 20,000 za watu waliokutwa na ugonjwa huo ikiwemo vifo 271 tangu ugonjwa huo uanze kusambaa dunia nzima.

Rwanda imekuwa miongoni mwa nchi za Afrika zenye mashariti magumu katika kujikinga na Covid 19 ikiwemo kuweka sheria ya kuwafungia wananchi wake ndani (lockdown) Machi 2020 ili kuzuia kazi ya maambukizi ya ugonjwa huo.
Aidha, Jiji la Kigali lilipigwa lockdown mwezi Januari kwa wiki mbili baada kubainika kuongezeka kwa maambukizi hayo.
Katika Ukanda wa Afrika mashariki, Rwanda, Kenya na Uganda wameshaanza kuchanja wananchi wake kuhusu Corona. Ethiopia, ambayo inamaambukizi machache zaidi Barani Afrika itaanza kutoa chanjo kesho Jumamosi.