×

Rais Samia Amewataka Wanaowaza 2025 Wasahau – Video

 

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema katika mabadiliko ya wizara aliyoyafanya aliangalia sifa za mtu katika sekta husika ambapo Prof. Palamagamba Kabudi ambaye ni mbobezi wa sheria, amemweka Wizara ya Sheria na Katibu, Dkt. Mwigulu Nchemba ni mchumi, amemweka Wizara ya Fedha.

 

Mama Samia amesema hayo leo Ijumaa, Aprili 1, 2021 katika Ikulu ya Chamwino Dodoma kwenye hafla ya uapisho wa Katibu Mkuu Kiongozi, mawaziri nane na manaibu waziri nane.

 

“Serikali hii ni moja tu, wote tunafanya kazi serikali moja, sekta yoyote uliyopo na hakuna haja ya kugombana na kunapotokea hilo kwa mawaziri na makatibu wakuu, kaeni muone jinsi mtakavyoweza kulimaliza. Kaeni mfanye kazi kwa pamoja.

 

 

Rais Samia Suluhu amewataka viongozi kuacha hili na lile kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025. Amewataka kufanya kazi na mambo ya mwaka 2025 yatajulikana muda ukifika. “Najua mwaka 2025 ni karibu, niwaambie tu jicho langu hili litaangalia sana, rekodi yako itakubeba, nawaomba sana kila mtu mwenye nia ya 2025 aache mara moja.

 

 

“Ndugu zangu mawaziri na manaibu Waziri, jahazi hili iwe upepo mdogo au upepo mwingi, linatakiwa kufika. Weledi katika kukata upepo kunahitajika sana. Ninatarajia kusikia kila waziri yuko sehemu yake akifanya kazi baada ya bunge la Bajeti.

 

 

“Wanawake wanafanya vizuri katika michezo hawasifiwi ila wanaume wanasifiwa hata kama hawajafika fainali, nakuomba Naibu waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul ukafanye kitu.

 

 

“Mnafanya wafanyabiashara kukimbia na kwenda sehemu nyingine,naomba mkaangalie suala la ulipaji wa kodi ukawe rafiki kwa kila mtu ili kupata mapato. Kuna waliokosa hizi nafasi kutokana na rekodi zao, nitakuwa na jicho kubwa sana kuwaangalia hata kama limelegea. Makatibu wakuu mmepoa. Zamu yenu siyo leo, ila inakuja.

 

Aidha, Rais Samia Suluhu amewataka viongozi kuacha kukusanya kodi kwa kutumia mabavu ikiwemo kufunga biashara za watu kisa wanadaiwa kodi.. Amesema licha ya kuwa sheria zinawaruhusu, lakini wakifunga biashara, wafanyabiashara hao wanahamia nchi jirani, hivyo kuikosesha serikali mapato.

 

Leave a Comment