
LICHA ya kwamba kila mwanadamu ataonja umauti kama maandiko ya vitabu vya dini yanavyoeleza, lakini katika kipindi cha mwaka 2019 na kuanzia Januari hadi Mei mwaka 2020, idadi kubwa ya vifo vya watu maarufu wa kada mbalimbali imeshika kasi na kuitikisa Tanzani na kuweka rekodi ya miezi 18 isiyosahaulika.
Hatua hiyo imekuja katika kipindi hiki ambacho pia kumeibuka wimbi la vifo vya ghafla ambavyo watalaam wa afya wanahusisha na magonjwa yasiyoambukiza kama vile moyo, shinikizo la damu, kisukari na matatizo ya figo.
Watalaam wa afya wanaeleza kuwa, kuongezeka kwa matumizi ya mitandao ya kijamii, kumesababisha taarifa za vifo hivyo kusambaa kama moto wa kifuu kuliko miaka yote.
Vilevile wamebainisha kuwa, mabadiliko ya mfumo wa maisha kwa Watanzania, ni moja ya sababu zinazochangia kuongezeka kwa vifo vingi vya ghafla tofauti na miaka iliyopita.
Sababu hizo zinalandana na ongezeko la vifo hivyo vya viongozi wa dini, siasa, uchumi, afya na jamii kwa jumla hali ambayo imeibua taharuki hasa ikizingatiwa kuwa dunia nzima imekumbwa na janga la Corona ambalo nalo limeshauwa idadi kuwa ya watu wengi duniani, ambapo inaelezwa hadi sasa zaidi ya wati milioni moja wameshafariki duniani kote!
Hakika sisi sote ni wa kurejea kwa Mungu!