×

Mtambo wa Nyuklia Iran Washambuliwa

MAELFU ya mashine zinazotumika kurutubisha nyenzo za nyuklia zimeharibiwa katika shambulio lililotokea kwenye mtambo muhimu, Jumapili, maafisa wa Iran wamesema.

Alireza Zakani, mkuu wa kituo cha Utafiti cha Bunge la Iran, amesema shambulio hilo “limeondoa” uwezo wa Iran wa kutekeleza mchakato huo.

 

Shambulizi hilo limetokea katika mtambo ulio mita 50 chini ardhi, afisa mwingine amesema.

 

Iran imelaumu Israel kwa kile ilichokiita kitendo cha “ugaidi wa kinyuklia”.

Israel bado haijathibitisha wala kukanusha madai hayo, lakini kituo cha redio cha Israel kinachomilikiwa na serikali kimenukuu vyanzo vya kijasusi vikisema ilikuwa operesheni ya kimtandao ya Mosaad.

 

Iran imesema itabadilisha mashine zilizoathirika – zile zinazotumika kuimarisha au kurutubisha, kemikali ya urani inayotumika katika uzalishaji wa nishati ya nyuklia au mabomu ya nyuklia – na hata kuweka mashine za kisasa zaidi.

 

Pia, Jumatano imetangaza kuwa itaongeza kiwango chake cha urutubishaji – kutoka asilimia 20 hadi 60.

 

Kiwango hicho kimekatazwa chini ya mkataba wa makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015, huku asilimia 60 ikiwa karibu sana na asilimia 90 inayohitajika kutengeneza silaha za nyuklia.

Leave a Comment