Jeshi la Polisi Mkoani Manyara, linamsaka Pascal Fisoo, mkazi wa Kijiji cha Soraa, Babati mkoani Manyara ambaye ni dereva bodaboda kwa kosa la kumbaka mwanafunzi wa kike mwenye umri wa miaka 15, anayesoma katika SHule ya Sekondari ya Kwang iliyopo Babati.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Paul Kasabago, amesema tukio hilo limetokea majira ya asubuhi ambapo mwanafunzi huyo akiwa na mwenzake, wakiwa wanaelekea shuleni, walikutana na dereva bodaboda huyo aliyesimama na kuwaomba kuwapa lifti.
Kamanda Kasabago anasema wanafunzi hao walipanda kwenye pikipiki hiyo lakini mita chache mbele, dereva huyo alibadili mwelekeo na kuingia kichakani, akasimamisha bodaboda na kutoa sime kuwatisha wanafunzi hao ambapo mmoja alifanikiwa kutoroka na kwenda kutoa taarifa huku bodaboda huyo akimbaka yule aliyesalia na alipomaliza, alikimbia na kuitelekeza pikipiki yake iliyokuja kuchukuliwa baadaye na polisi.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mji wa Babati, Frank Mchuno amethibitisha kumpokea mwanafunzi huyo na kumkuta na majeraha mengi kwenye mwili wake ikiwemo sehemu za siri na kisha kumpatia dawa za kuzuia maambukizi.