
KIDA Kudz -rapa maarufu kutoka Nigeria mwenye makazi yake jijini London, Uingereza, amerejea kwa kasi kwenye gemu baada ya kutoa wimbo wake mpya uitwao Animalistic.
Wimbo huo unapatikana kwenye majukwaa yote ya ‘ku-stream’ muziki mitandaoni na tayari umeanza kuwa gumzo kutokana na ufundi uliotumika kuusuka wimbo huo, ukihusisha vionjo vya Afrobeat na Afro Jiggy vinavyopendwa zaidi.

Akizungumzia wimbo huo, Kida amesema: “Kuandika wimbo wa Animalistic lilikuwa ni jambo la kiroho kwangu. Niliamka asubuhi moja, nikachukua kalamu na karatasi na kuanza kuandika kile kilichokuwa ndani ya kichwa changu; mashairi yakawa yanatiririka tu kutoka kichwani mwangu. Nilikuwa nikichora picha halisi yakijana wa Kiafrika akizungumza na watu wake, akijaribu kuwahubiria jambo kwa namna ya upole.”
Wimbo wa Animalistic unazungumzia mada kadhaa kuanzia kifo na hali ya kutoridhishwa na mambo yanayofanywa na jamii na uzinduzi wake unakwenda sambamba na uzinduzi wa video yake, iliyoongozwa na dairekta maarufu, iO Filmworks.

Ndani ya video hiyo, Kida anaonekana akirap ndani ya basi linalowaka moto, lililowabeba wafungwa ambao nyuso zao hazionekani huku Kida akiwa amesimama kwenye mti ambao ni nembo yenye maana kubwa iliyojificha.
“Unaweza kuwa unaburudishwa na wimbo huu lakini wakati huohuo unapata ujumbe mkubwa kuhusu masuala mbalimbali yanayowahusu vijana. Kuna stori ya kweli ndani ya wimbo huo ambayo ilitokea asubuhi ya siku niliyoandika mashairi yake,” anasema Kida.
Na Mwandishi Wetu