×

Shigongo Atembelea Wagonjwa Nyehunge, Awapa Neno Wahudumu wa Afya

MBUNGE wa Jimbo la Buchosa, Eric Shigongo akiambatana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Buchosa, Crispin Luanda wametembelea wakina mama ambao wamepatiwa mafunzo ya chakula bora katika Zahanati ya Nyehunge ikiwa ni moja ya mikakati ya Jimbo la Buchosa kuondoa tatizo la utapiamlo kwa watoto chini ya miaka mitano katika halmashauri hiyo.

Shigongo amewataka wakina mama hao ambao wamepatiwa mafunzo kuyafuata na kutoa elimu kwa wengine ili jamii ya watu wa Buchosa waondokane na utapiamlo kwani vyakula vya kuongeza virutubisho vipo vya kutosha hivyo ni vyema elimu ikaendelea kutolewa kwa wananchi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Crispin Luanda amesema mafunzo hayo ni mpango mkakati wa kuhakikisha wanaondoa utapiamlo kwa watoto chini ya miaka mitano kwa kutoa elimu kwa wakina mama wenye watoto wadogo namna ya kuandaa chakula lishe.

 

Aidha, Ofisa Lishe wa Halmashauri hiyo Benedicta Peter amesema wameweka utaratibu wa elimu pamoja na kuwapa lishe bora watoto wenye utapiamlo kwa kuwapa vyakula vyenye vitamini vyote.

Shigongo pia ametembelea wagonjwa katika Zahanati ya Nyehunge na kuwajulia hali akiwa kwenye ziara yake katika maeneo mbalimbali ya Jimbo hilo.

 

Shigongo amezungumza na wagonjwa hao ambapo wamemweleza baadhi ya changamoto zilizopo kwenye zahati hiyo na kuahidi kuzitatua changamoto hizo.

Shigongo amezungumza na watumishi wa Zahanati ya Nyehunge na kuwaeleza umuhimu wa kutoa huduma na kauli nzuri kwa wagonjwa wanaowahudumia ikiwa ni pamoja na kuwapa ushauri mzuri kulingana na ugonjwa wa mtu.

 

Shigongo amesema hiyo itasaidi wananchi kufurahia huduma na wahudumu wa Zahanati hiyo huku akisisitiza kuwa hatakuwa tayari kuona muhudumu wa afya anamnyanyasa mwananchi ambaye ameenda kwa ajili ya kupata huduma kulingana na matatizo yake ya kiafya.

“Ninawaomba watumishi wenzangu fanyeni kazi kwa moyo mmoja kuwahudumia wananchi wetu kwa kutoa huduma na kauli nzuri kwa wagonjwa vinginevyo Mimi sitokubali kuona mwananchi ananyayasika katika Jimbo langu kwa kupewa huduma zisizoridhisha na kauli mbaya kutoka kwenu wahudumu wa afya tuwasaidie wananchi wetu na tuwepe ushauri mzuri wa kiafya ili tujenge jamii inayodhaminiana,” alisema Shigongo.

Leave a Comment