
KAMPUNI ya Vodacom Tanzania imezindua Tovuti ya E-Fahamu, ambayo ina lengo la kuwasaidia watoto na walimu kupata vitabu vya kiada na ziada kwa njia ya kidijitali bure.
Aidha Vodacom imeshirikiana na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), kuweka vitabu na mitaala iliyopitishwa na TET kwenye mfumo huo Ikiwa ni nakala zaidi ya 80 za machapisho ya kiada, nakala zaidi ya 1,020 za machapisho ya ziada, na katuni 18 zenye masomo.
Akizindua mfumo huo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, aliishukuru Vodacom kwa kuja na ubunifu huo iliyolenga kuboresha hamasa ya Wanafunzi kujisomea, Jambo ambalo litawafanya kufanya vizuri katika mitihani yao.
“Kama tunavyojua watoto wetu wanapenda kuchezea simu, sasa badala ya kuangalia mambo yasiyofaa, Sasa Vodacom Tanzania PLC imewapa fursa ya kupata maudhui ya masomo, na kubwa ni kuwa maudhui haya yatapatikana bure hivyo watoto wa hali zote za kiuchumi watanufaika, nawapongeza sana kwa hili.”
Prof. Ndalichako alipongeza juhudi zinazofanywa za kuwafikia wanafunzi wengi hususani wa vijijini kwa Vodacom Tanzania Foundation kushirikiana na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kugawa kompyuta na vipanga njia (routers) kwa shule za sekondari nchini.
Mpaka Sasa Komyuta 48 na vipanga njia 24 pamoja na Sim Card zimetolewa kwa shule za sekondari 24 Katika awamu ya kwanza wakati awamu ya pili wamepanga kuzifikia jumla ya shule za sekondari 163, na kwamba tayari shule 151 zimefikiwa kwenye mikoa mbalimbali nchini na kutoa kumpyuta 556, printer 83 na vipanga njia 151 ikiwa na lengo la kuwanufaisha wanafunzi na waalimu 4,000.
“Tunawashukuru sana kuweza kuleta tabasamu kwa wanafunzi wetu, hususan waliopo maeneo ya vijijini.”
Alisema ni imani yake kuwa kupitia jukwaa la E-Fahamu ufaulu utaongezeka kwa sababu walimu na wanafunzi watakuwa na uwezo wa kupata maudhui mbalimbali, hivyo kujiongezea maarifa yatakayowawezesha wanafunzi kufaulu mitihani yao katika ngazi mbalimbali.
“Nawaomba Vodacom Tanzania Foundation muendelee kuongeza idadi ya vitabu katika jukwaa hili ili kuongeza wigo kwa walimu na wanafunzi kupata maudhui mengi zaidi, na hivyo kusaidia katika kujifunza masomo mbalimbali. “
Prof. Ndalichako alitumia fursa hiyo kutoa rai kwa kampuni nyingine kuiga mfano wa Vodacom Tanzania, kupitia taasisi yake ya uwajibikaji kwa jamii ili kuhakikisha kwamba wanaiunga mkono Serikali katika ajenda yake ya kuhakikisha wanafunzi wanakuwa na mazingira mazuri ya kupata elimu bila gharama yoyote.
Awali, Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Foundation, Rosalynn Mworia, alisema mfumo huo ambao zamani ulijulikana kama Instant Schools, umeongeza maudhui kutoka TET ili kuweza kupata matokeo chanya zaidi kwa wanaosoma kwa mfumo wa Kiswahili na Kiingereza.
“Kupitia jukwaa hili mtu yeyote anaweza kutafuta, kupakua na kupata maudhui mbalimbali ikiwemo yale ya elimu ya darasani na stadi za kazi kupitia mtandao wa Vodacom kwa kutembelea tovuti ya “
“Lengo letu kuu ni kutumia mtandao wetu wa mawasiliano ili kuboresha maisha ya watu wote kupitia sekta ya elimu, tumefanya kazi pamoja na wadau mbalimbali wa elimu kama vile TET, na mfuko wa UCSAF katika kufikia wanuafunzi kwenye shule za sekondari, na pia na Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira katika kutengeneza maudhui ya uhifadhi wa mazingira ili kueneza ufahamu na kusambaza elimu juu ya mazingira.
Alisema mpaka sasa wanufaika wako zaidi ya 150,000 kwenye mtandao. Alibainisha orodha ya vitabu kutoka TIE ambavyo wanafunzi na walimu wa shule za msingi na sekondari wanaweza kupata kwenye mfumo kwa wanafunzi wa darasa la Saba ambao watapata vitabu vya Hisabati, Masomo ya Jamii, Sayansi na teknolojia, Stadi za Maisha,na Uraia na Maadili.
Alisema kwa upande wa darasa la Sita, vitabu vinavyopatikakana ni Hisabati wakati wale wa darasa la 3, 4 and 5 ni vitabu vya masomo ya Kiswahili, Kiingereza, Hisabati, Uraia na Maadili kutoka TIE.
Kwa upande wa darasa la 1 na 2 ni vya somo la kujifunza stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu na somo la afya na mazingira.
“Pia E-fahamu ina vitabu vya Jiografia na Historia kwa wanafunzi wa sekondari wa kidato cha kwanza na cha pili na wanafunzi wa Sekondari ( O na A-Level) vitabu vinavyopatikana ni Basic Applied Mathematics, Biology, General Chemistry, Physics na Kiswahili.
. Alisema E-fahamu pia ina nyenzo kubwa ya elimu kutoka washirika wa hapa nchini, Taasisi ya Shule Direct pamoja na wale wa kimataifa.
“ Elimu inayopatikana ni pamoja na Hisabati, Sayansi, Fizikia, Kiswahili na Kiingereza, yote haya yanapatikana katika mifumo ya maandishi yaani PDF, video, picha na mazoezi.
“ Wanaopenda kusoma hadithi pia watazitapata kwenye E-fahamu. Walimu na watu wazima wanaotaka kuendeleza ujuzi wao, watafaidi channeli mbalimbali ikiwemo ile ya Tessa kwa walimu, Sikana, Thoughful learning, Khan University, HP Life courses na nyinginezo nyingi.”
“ Hii siyo mara ya kwanza kwa Vodaocom kutumia teknolojia na tehama kuendeleza elimu nchi, huko nyuma tuliingia ubia na kampuni ya Samsung kutoa vifaa vya tehama kwa shule tano za Dar es Salaam ambapo wanafunzi zaidi ya 4,000 walinufaika na masomo ya tehama.
Aidha, aliishukuru Serikali kwa kuwapa nafasi ya kutumia maudhui yaliyopitishwa kutoka TIE, pia alitoa rai kwa hivyo wadau wengine wenye maudhui yaliyoruhusiwa wajitokeze ili kuhakikisha E-fahamu inakuwa na maudhui ya kutosha, ili iweze kusaidia juhudi za serikali katika kutoa elimu bora zaidi bila gharama yoyote