
KOCHA Mkuu wa Klabu ya Simba, Didier Gomes amesema kuwa bado ana imani kubwa kuwa kikosi chake kinaweza kupindua meza, na kupata ushindi kwenye mchezo wao wa marudiano dhidi ya Kaizer Chiefs na kufanikiwa kutinga Hatua ya Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Simba, juzi Jumamosi wakicheza kwenye Uwanja wa FNB ‘Soccer City’ na walikutana na kipigo cha mabao 4-0 ugenini dhidi ya Kaizer, matokeo ambayo yameweka rehani nafasi yao ya kutinga hatua inayofuata.
Kwa matokeo hayo Simba sasa wana mlima mrefu wa kupanda kwa kuhakikisha wanashinda mabao 5-0 kwenye mchezo wa marudiano, unaotarajiwa kuchezwa Jumamosi ijayo kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Gomes alisema: “Jambo lolote linawezekana kwenye mpira, hatujafurahia matokeo lakini bado tuna matumaini, ni muhimu sana kuamini kwamba tunaweza kubadili matokeo, lakini ni lazima tuwe bora zaidi.
”Alipotafutwa mwenyekiti wa zamani wa Simba na mwanachama maarufu wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage alisema:“Kwenye mpira jambo lolote linaweza kutokea, hakuna anayeweza kupinga hilo.
Simba iliwahi kufungwa mabao 4-0 nyumbani dhidi ya Mufulira Wanderes, lakini wakapindua meza ugenini kwa kuwafunga mabao 5-0, hivyo lolote linaweza kutokea.“Lakini tunapaswa kukubali ukweli kuwa Kaizer walikuwa bora kuwazidi Simba, na tulifanya makosa mengi hasa katika safu ya ulinzi jambo ambalo ni lazima tulifanyie kazi kuelekea mchezo wa marudiano.”
STORI NA JOEL THOMAS | GPL