
BAADA ya wachezaji wa Klabu ya Yanga kupewa mapumziko ya siku nne, mastaa wa timu hiyo akiwemo Yacouba Songne na Mukoko Tonombe wametimka baada ya kuitwa kwenye timu zao za taifa.
Wachezaji hao ambao wamekuwa kwenye kiwango bora tangu wajiunge na Yanga mpaka kufikia hatua ya kuitwa kutumikia timu zao za taifa.Kwa upande wa Yacouba raia wa Burkina Faso, ambaye alijiunga na Yanga mwanzoni mwa msimu huu ni mara yake ya kwanza kuitwa ndani ya kikosi hicho.

Akizungumza na Championi Jumamosi, Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alisema kuwa: “Wachezaji wamepewa siku nne kwa ajili ya mapumziko na baada ya hapo watarejea kambini Jumatatu.
“Tumewaruhusu wachezaji wawili walioitwa kwenye timu zao za taifa ambao ni Yacouba Songne na Mukoko Tonombe.“Yacouba tayari ameondoka lakini kwa upande wa Mukoko ataondoka kesho (leo), lakini yeye hataenda Congo bali atajiunga nayo moja kwa moja Tunisia,” alisema Bumbuli
STORI: LEEN ESSAU, Dar es Salaam