



KAMISHNA wa Wizara Ya Ardhi, Nyumba Na Maendeleo Ya Makazi Kanda ya Dar es Salaam Bw. Idrisa Kayera ametoa wito kwa wananchi kulipia hati za Viwanja vyao ili waweze kupatiwa.
Akizungumza katika zoezi la ugawaji hati lililofanyika kata ya kibwegele-kibamba wilaya ya Ubungo jijijni Dar es Salaam, Kayera amesisitiza kuwa zoezi la upatikanaji wa hati za Viwanja kwa sasa ni rahisi zaidi ambapo mwananchi anaweza kupata hati yake ndani ya siku mbili baada ya kukamilisha malipo na taratibu zote za kiwanja husika.
Kayera pia ametoa rai kwa makampuni yanayojihusisha na upimaji na urasimishaji wa viwanja kwa wananchi kufanya kazi kwa weledi na uhakika ili wananchi wapate hati zao mapema kama ambavyo wizara ya Ardhi na Serikali zimeelekeza juu ya umilikishwaji wa Viwanja kwa wananchi.
Kamishina Kayera ambaye aliambatana na maafisa wengine kutoka Wizara Ya Ardhi, Nyumba Na Maendeleo Ya Makazi amesema zoezi hilo la ugawaji hati litakua endelevu na wataendelea kuzunguka maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam.