
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema ameteua asilimia 46 ya Makatibu Tawala Wanawake hivyo anataka kuona utofauti katika Utendaji badala ya kuendekeza majungu kazini.
Samia amesema hayo leo Jumatano, Juni 2, 2021 wakati akiwaapisha Makatibu Tawala wa Mikoa na viongozi mbalimbali aliyowateua hivi karibuni, katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma na kuwataka wawe watiifu kwa viongozi na wananchi.

“Makatibu Tawala wa Mikoa mnakwenda kuwa watendaji wakuu wa mikoa, wakuu wa sekretarieti za mikoa na makatibu wa kamati za usalama za mkoa, mna kazi kubwa ya kwenda kufanya huko muendako, watendaji wote wa mikoa wako chini yenu.
“Nimewaweka wanawake asilimia 46 kwa maksudi, ninafahamu wanawake mna uwezo mkubwa wa kusimamia kazi. Tumeona walipokuwa Ma-RAS wengi wengi wanaume hawakufanya vizuri sana, sasa hivi mmekaribia kulingana, tunaamini nyie mtaweza, mkishindwa basi tena.
“Kwa mikoa ambayo kuna wanawake kwa wanawake, ile ‘Bibi usinibabaishe’ nisiisikie, pale nyinyi sio wanawake ni mkuu wa mkoa na RAS wako, hakuna sababu ya kuparurana, mkifanya hivyo mtaniabisha mimi, yakayosemwa ndio tabia za wanawake, mbona mnaolewa pamoja.











“Muende mkachape kazi wanawake kwa wanawake, hiyo mikoa naitegemea sana, nione impact ya kuweka wanawake pamoja, kazi ziende, spidi iende, nataka kuona hayo matokeo,” amesema Rais Samia.